Athari za Mimba za Utotoni kwa Afya ya Umma na Ustawi wa Vijana (Umri wa Miaka 10-19)

Na Angela Kibwana, Morogoro

Sera ya Afya ya mwaka 2007 inasisitiza na kuelekeza umuhimu wa kuwapa vijana taarifa, elimu, na huduma za afya zinazofaa, ikijumuisha afya ya uzazi inayokidhi mahitaji maalum ya kiumri bila ubaguzi kama ilivyo kwa makundi mengine ya kijamii.

Miongoni mwa masuala muhimu ambayo vijana wanapaswa kufundishwa ni namna ya kukabiliana na mabadiliko ya mwili wakati wa balehe, kama vile jinsi ya kudhibiti tamaa za kingono, jinsi ya kuepuka mahusiano ya mapema, na namna ya kujikinga dhidi ya mimba za mapema.

Uwezeshaji huu ni muhimu katika kuimarisha afya chanya, matokeo ya kijamii, kisaikolojia, kiakili, kihisia, na kiroho kwa vijana.

Moja ya sababu kuu za kutoa taarifa, elimu, na huduma kwa vijana, kama ilivyoelezwa kwenye sera ya afya ya uzazi, ni kupunguza changamoto za afya ya uzazi miongoni mwa vijana, ikiwemo mimba za mapema.

Changamoto hii inaangaziwa kwenye Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs 2030, Malengo 3 na 5), Ajenda ya Kitaifa ya Kuwekeza katika Afya na Ustawi wa Vijana (NAIA-AHW 2021/2022 na 2024/2025), na sera zingine za kitaifa.

Kwa mfano, Sheria ya Mtoto (Tanzania) – 2009 inalinda haki za watoto, ikijumuisha haki ya elimu, afya, na ulinzi dhidi ya aina zote za unyanyasaji wa kisaikolojia au kimwili. Mimba za utotoni mara nyingi huhusishwa na ukiukwaji wa haki za wasichana.

Kifungu cha 5 kinabainisha haki za watoto, ikiwemo haki ya elimu. Kifungu cha 13 kinajadili ulinzi wa watoto dhidi ya vurugu, jambo linalochangia kwa kiasi kikubwa kwenye ndoa na mimba za mapema.

Aidha, Kifungu cha 16 kinahusu haki ya huduma bora za afya, inayohusiana moja kwa moja na elimu ya afya ya uzazi na huduma kwa vijana, inayolenga kuwakinga dhidi ya mimba za utotoni.

Licha ya kuwepo kwa sera, sheria, mipango na huduma mbalimbali, mimba za utotoni zinaendelea kuwa changamoto kwa afya ya jamii, maendeleo ya kiuchumi, na ustawi wa jumla wa vijana na vizazi vyao.

Kitaifa, kiwango cha mimba za utotoni (umri wa miaka 10-19) kimepungua kutoka asilimia 27 hadi 22, wakati katika mkoa wa Morogoro kimepungua kutoka asilimia 39 hadi 28 Kwa mujibu wa Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania (TDHS) ya mwaka 2015/16 na 2022.

Sababu zinazoendelea kuchangia uwepo wa mimba za utotoni ni pamoja na ukosefu wa upatikanaji wa taarifa sahihi za afya ya uzazi kutoka kwenye vyanzo vinavyotegemewa, unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto, ndoa za utotoni, desturi zinazozuia upatikanaji wa elimu na taarifa sahihi, changamoto za kupata huduma rafiki kwa vijana, malezi duni, na umaskini.

Mimba za utotoni huathiri vijana wa kike na wa kiume kwa njia mbalimbali, ikijumuisha changamoto za kisaikolojia na afya ya akili, kuacha shule, kulazimishwa kuingia kwenye ndoa za utotoni, kutengwa kijamii, na kuachwa na wenza wao, kushindwa kuwalea watoto, lishe duni, kuongezeka kwa uhalifu, unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto, na ongezeko la vifo vya mama na watoto wachanga.

Mwandishi wa makala haya alipata fursa ya kuzungumza na wadau mbalimbali kuhusu changamoto za mimba za utotoni, ambapo walitoa simulizi zao binafsi zinazodhihirisha uzito wa tatizo hili:

Mariam John (si jina lake halisi), msichana wa miaka 16, alisema, “Nilikuwa na ndoto nyingi, kama kuwa daktari ili kusaidia watu na kuleta mabadiliko katika jamii yangu. Nilijitahidi kusoma na nilipenda kujifunza. Hata hivyo,ndoto zake ziliyeyuka alipogundua kuwa ana mimba.

“Nililazimika kuacha shule nikiwa kidato cha kwanza, na hapo ndipo maisha magumu na ya huzuni yalianza; nilipoteza marafiki na matumaini ya maisha bora.”

Simulizi hili linaakisi hali halisi ya wasichana wengi wanaokumbwa na changamoto ya mimba za utotoni, Mara nyingi wanapoteza fursa za kielimu huku wakikabiliana na changamoto za afya, kijamii, na kiuchumi zinazozuia ndoto na mustakabali wao.

Joseph Pius (si jina lake halisi) kutoka Mwembesongo, Morogoro, alishiriki ushuhuda wake: “Sikuwa na elimu kuhusu afya ya uzazi nilipokuwa kwenye mahusiano ya kingono na msichana aliyekuwa mfanyakazi wa nyumbani kwa jirani. Baada ya uhusiano huu, alipata ujauzito, na marafiki zangu walinipa ushauri potofu wa kumshawishi kutoa mimba. Alikubali kutoa ujauzito huo kwa njia isiyo salama, na baada ya hapo alipatwa na matatizo makubwa, akapoteza kazi na afya yake ikaharibika. Uhusiano wetu uliisha, na hadi sasa sijui yuko wapi na anaendelea vipi.”

Pius alikumbana na migogoro ya kifamilia na hata kufungwa kwa muda kutokana na tatizo hilo, jambo lililomwacha na aibu na kujutia. “Nilijuta kila siku. Marafiki waliniacha, na nilijikuta nimejitenga. Sasa nawashauri marafiki zangu kuepuka tabia hatarishi kama mahusiano ya mapema na ngono zisizo salama na kuwaunganisha na waelimishaji rika wa afya ya vijana.”

Ili kukabiliana na changamoto hizi za afya ya uzazi kwa vijana, ikiwemo mimba za utotoni, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Mtandao wa Haki za Uzazi kwa Wanawake Afrika (WGNRR) na Chama cha Uzazi na Malezi Bora Tanzania (UMATI) wanaendesha mradi wa Voice of Youth, unaofadhiliwa na Amplify Change kutoka Uingereza.

Mradi huu unalenga kushawishi wadau mbalimbali kitaifa na kimataifa kuhakikisha utekelezaji madhubuti wa sera, sheria, na miongozo inayoboresha afya ya uzazi na ustawi wa vijana.

Utekelezaji wa sera hizi unatarajiwa kuboresha upatikanaji na matumizi ya huduma za afya ya uzazi rafiki kwa vijana bila ubaguzi, kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo, na kuhakikisha mustakabali mzuri wa taifa letu.

Kwa mujibu wa Evans Rwamuhuru, Meneja wa Mradi wa Voice of Youth kutoka UMATI, alisema kupitia juhudi zao za ushirikiano wamefundisha watoa huduma za afya 36, waandishi wa habari 10, na waelimishaji rika 30 katika mikoa ya Morogoro na Iringa, kwa lengo la kuwafikia vijana kupitia njia mbalimbali.

Ifikapo mwisho wa mradi, unatarajiwa kuwafikia vijana 59,400 ndani ya miaka miwili (Januari 2023 hadi Desemba 2024).

Kufikia Septemba 2024, tayari walikuwa wamewafikia vijana 222,674 katika mikoa ya Morogoro na Iringa kupitia vituo vya utoaji huduma za afya, huduma za nje ya vituo, kliniki za wikendi, waelimishaji rika, na vyombo vya habari.

Katika Mkoa wa Morogoro mradi uko katika Halmashauri  ya Mlimba wilayani Kilombero wamefikiwa vijana 26,854, Kilosa vijana 31,053, Morogoro Manispaa 114,207, Manispaa ya Iringa 40,830, na Kilolo vijana 9,730.  

Michael Mbele, Afisa wa Programu kutoka Wizara ya Afya, anasisitiza umuhimu wa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana ambapo Serikali inasisitiza hili kupitia miongozo yake na kuhakikisha kuwa wale walioko shuleni wanapata elimu inayozingatia miongozo hii. Wanaelekeza vijana kujiepusha na ngono ili kuzuia mimba za utotoni.

Catherine Thobias Madaha, Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto wa Mkoa (RRCHCo) kutoka ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, alieleza kuwa kiwango cha mimba za utotoni katika mkoa wa Morogoro kimepungua kutoka asilimia 39 hadi 28 (2015/16 hadi 2022), upungufu wa asilimia 11.

Kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo,ikiwa ni pamoja na UMATI na WGNRR Afrika, mkoa unafanya kazi kwa bidii kupunguza tatizo la mimba za utotoni.

Alisema kuwa kupata ujauzito katika umri mdogo kunaleta athari za kiafya, kwani kinamama wanapaswa kufikisha umri wa miaka 20 ili mifumo yao ya uzazi iweze kukomaa ipasavyo.

Licha ya juhudi zinazoendelea za kupunguza mimba za utotoni katika mkoa wa Morogoro, mila na desturi, hasa katika wilaya kama Gairo ambako ndoa za utotoni ni nyingi, huchangia sana katika kuendeleza changamoto hii.

Pia, Bi Catherine alisema, “Kama wataalam wa afya, hatutoitoi tu matibabu bali pia elimu, tunawahimiza vijana kutafuta huduma za afya rafiki badala ya kutegemea taarifa za mtaani. Wale wanaoshindwa kustahimili shinikizo wanaweza kushauriwa kusubiri hadi watakapokuwa na umri mzuri wa kufanya maamuzi sahihi kuhusu maisha yao ya baadaye.”

Lengo letu kama mkoa (Morogoro) ni kuimarisha ushirikiano na washirika wa maendeleo kupunguza kiwango cha mimba za utotoni kutoka asilimia 28 hadi chini ya asilimia 10, kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto za kiafya za vijana.

Kwa kupitia ushirikiano wa pamoja na juhudi za kudumu, tunaweza kujitahidi kuboresha mazingira ya afya ya uzazi kwa vijana, kuhakikisha maisha bora kwao na jamii zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *