Na Angela Kibwana, Morogoro
Askofu wa Jimbo Katoliki Morogoro, Mhashamu Lazarus Msimbe SDS, ametangaza kuwa ukarabati wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Patris ni sehemu muhimu ya mpango mkakati wa miaka mitano wa jimbo hilo.
Mpango huu unalenga maandalizi ya kusherehekea Jubilei ya Miaka 75 ya Jimbo Katoliki Morogoro ifikapo mwaka 2028.
Katika mahojiano maalum, Askofu Msimbe alieleza kuwa ukarabati huo una nia ya kuboresha muundo wa zamani wa kanisa hilo na kulifanya kuwa na mwonekano wa kisasa, unaoendana na hadhi ya nyumba ya Mungu.

Mpango huo ni sehemu ya safari ya kiroho kwa waamini kuelekea Jubilei, akisisitiza umuhimu wa waamini kushiriki si tu katika ukarabati wa kanisa, bali pia ukarabati wa roho zao.
Sababu za Ukarabati
Askofu Msimbe alifafanua kuwa maamuzi ya kukarabati Kanisa Kuu la Mtakatifu Patris yametokana na hali ya uchakavu wa miundombinu yake, tofauti na makanisa mengine mazuri zaidi ndani ya jimbo hilo.
Aliongeza kuwa, licha ya umuhimu wa kihistoria wa Kanisa hilo lililojengwa mwaka 1961, mtindo wake wa awali hauonekani kama Kanisa, jambo ambalo limesababisha watu kulichanganya na ukumbi au ghala.
Mbali na hilo, Askofu Msimbe alibainisha kuwa ukarabati huu pia unahitajika kutokana na mvua zinazovuja ndani ya kanisa, hata katika sehemu anapokaa askofu. “Niliona ni muhimu kuhakikisha usalama wa kanisa lote kwa kubaini maeneo yote yenye matatizo kabla ya kutoa tamko la ukarabati,” alisema.
Aidha, ukarabati huu ni sehemu ya maandalizi ya kusherehekea miaka 75 tangu kuanzishwa kwa Jimbo Katoliki Morogoro mwaka 1953, baada ya wamisionari wa kwanza kuanzisha Ukristo katika eneo hilo mwaka 1868.

Hatua za Ukarabati
Askofu Msimbe alieleza kuwa mchakato wa ukarabati umegawanyika katika hatua kuu tatu:
- Kubadilisha sura ya mbele ya kanisa: Hatua ya kwanza ni kuboresha mwonekano wa mbele wa kanisa kwa gharama ya shilingi milioni 130.
- Kurekebisha paa: Mabati yote ya zamani yanayovuja yameondolewa, na tayari kazi ya kuezeka paa jipya imeanza.
- Uboreshaji wa ndani: Mwonekano wa ndani wa kanisa unaboreshwa, pamoja na kuhamisha Tabernakulo kutoka pembezoni mwa kanisa na kuiweka mahali pa wazi ambapo waamini wote wataweza kuiona.
Changamoto na Suluhisho
Ukarabati huu umesababisha shughuli za ibada kuhamishiwa kwenye kituo cha mafunzo cha Social Education Centre kilicho karibu na Kanisa Kuu. Ili kuboresha huduma za kiroho, idadi ya misa imeongezeka ili kuhakikisha waamini wanasali kwa utulivu.
Kwa gharama inayokadiriwa kufikia zaidi ya shilingi milioni 600, juhudi za kuchangia fedha zinaendelea kushirikisha waamini, wadau, na serikali. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa mchango wa shilingi milioni 100 kufanikisha ukarabati huu.

Askofu Msimbe alihitimisha kwa kusema, “Tunataka Kanisa Kuu letu lionekane wazi kuwa ni nyumba ya Mungu. Tunaweka kumbukumbu za hatua zote za ukarabati, kuhakikisha historia yetu inalindwa.”
Mwisho
ReplyForwardAdd reaction |