Na Angela Kibwana
Watoto ni msingi wa kesho ya jamii na Kanisa, Hata hivyo, usalama wao mara nyingi uko hatarini kutokana na changamoto za kimazingira, kijamii, na kiroho. Katika jamii ya sasa, vitendo vya unyanyasaji wa watoto vinaendelea kuongezeka.
Ni jukumu la kila mwana jamii kujiuliza, je, anashiriki vipi katika kulinda watoto dhidi ya vitendo vinavyohatarisha usalama wao?
Mambo kama unyanyasaji wa kijinsia, ubakaji, na ulawiti yanaathiri ustawi wa watoto na yanahitaji mshikamano wa wazazi, walezi, viongozi wa dini, serikali,na wadau wa maendeleo, hivyo Ulinzi wa watoto si suala la hiari bali ni jukumu la msingi.
Kanisa na Ulinzi wa Watoto
Kanisa Katoliki limekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza maadili ya Kikristo. Kupitia mpango wa “Safeguarding of Children and Vulnerable Persons,” Kanisa linahimiza kuwapa watoto mazingira salama kwa ukuaji wao wa kimwili na kiroho.
Padri Nicholaus Difulata wa Jimbo Katoliki Morogoro, wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Watoto Mashahidi, alisema kuwa sherehe hiyo inakumbusha waamini na jamii jukumu lao la kuwajali watoto kama hazina ya jamii.

“Tunapowapa watoto mazingira salama, tunawajengea msingi wa maisha yenye matumaini, tunajenga jamii imara, na tunatimiza wito wa Kikristo wa kuwajali ‘wadogo hawa,’” alisema Padri Difulata.
Aliongeza kuwa dhana ya kila mtu kuwa mlezi wa watoto imepungua katika jamii ya sasa. Watu hawashirikiani kufuatilia masuala ya ulinzi wa watoto, jambo linalochangia changamoto kama watoto kukata tamaa na hata kupoteza maisha.
Serikali na Sheria za Ulinzi wa Watoto
Serikali ya Tanzania imeimarisha jitihada zake za kulinda watoto kupitia sheria na miongozo mbalimbali, kama Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009. Sheria hii inalinda haki za watoto dhidi ya unyanyasaji wa kimwili, kihisia, na kingono. Aidha, sheria hiyo inasisitiza haki za msingi za watoto kama elimu, afya, na ulinzi dhidi ya ajira za utotoni.
Kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali na taasisi za kimataifa kama UNICEF na Save the Children, serikali imeanzisha miradi ya kuimarisha ulinzi wa watoto.
Miradi hii inalenga kupambana na ukatili wa kijinsia na ajira za watoto, Hata hivyo, utekelezaji wake unakumbana na changamoto kama uhaba wa rasilimali na uelewa mdogo wa sera hizo ndani ya jamii.

Changamoto za Familia na Jamii
Padri Difulata alisisitiza kuwa baadhi ya changamoto zinazowakabili watoto zinaanzia ndani ya familia, ambapo Wazazi wengi wanashindwa kuwafuatilia watoto wao kwa umakini kutokana na majukumu ya kazi.
Alisema Malezi yameachiwa wafanyakazi wa nyumbani, hali inayochangia ongezeko la unyanyasaji kwa watoto.
“Watoto wengi wanakosa amani nyumbani na wanakimbilia mitaani kutafuta usalama,” alisema Padri Difulata. Aidha, watoto wengi wanalelewa na mzazi mmoja au hata bibi zao, jambo linaloathiri malezi yao kwa kiasi kikubwa.
Nafasi ya Jamii
Jamii ina jukumu kubwa katika kuimarisha ulinzi wa watoto hivyo ni muhimu kwa kila mtu kuona mtoto wa mwenzake kama mtoto wake mwenyewe.
Padri Difulata alitoa wito kwa jamii kutafuta amani kwa watoto kwa kuhakikisha wanapata malezi bora na mazingira salama.
“Tuwaombee watu wenye mioyo migumu ambao hawaoni thamani ya watoto kama zawadi kutoka kwa Mungu. Watoto ni hazina na Kanisa la kesho,” alisema.

Ulinzi wa watoto ni jukumu la pamoja linalohitaji mshikamano wa wazazi, walezi, serikali, viongozi wa dini, na wadau wengine, Kila mtu ana nafasi ya kuchangia kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama yanayowapa fursa ya kufikia ndoto zao.
Kwa kuzingatia miongozo ya Kanisa na sera za serikali, tunaweza kujenga jamii imara inayowajali watoto kama hazina ya kesho.