Na Angela Kibwana.
Katika kipindi kifupi cha miezi mitatu pekee, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umeandika historia kwa kulipa mafao ya jumla ya Shilingi bilioni 126 kwa wastaafu.
Hii si tu takwimu ya kifedha bali ni ushuhuda wa dhamira ya dhati ya mfuko huu katika kuimarisha maisha ya wastaafu waliolitumikia taifa kwa bidii na uadilifu.
Kwa wengi, kipindi cha kustaafu kinaweza kuonekana kama changamoto, lakini kwa msaada wa PSSSF, ndoto mpya zinaibuka katika kustawisha familia, jamii na mustakabali wa taifa.
Hifadhi ya jamii inasaidia kukuza mshikamano wa kijamii kwa kutoa uhakika wa msaada wa kifedha kwa watu waliolitumikia taifa kwa muda mrefu, Mfuko huu unaonyesha kuwa jamii inathamini mchango wa wazee, hivyo kukuza maadili ya heshima na utu kwa wastaafu.
Mfumo wa PSSSF, kwa mfano wake bora wa usimamizi na utekelezaji wa mafao, si tu umejenga imani miongoni mwa wastaafu na wanachama wake, bali pia umeonyesha umuhimu wa kuwa na mifumo imara ya hifadhi ya jamii.
Katika ulimwengu unaokumbwa na changamoto za kiuchumi, mfumo huu ni dira inayoonyesha jinsi taifa linaweza kujenga jamii yenye utu, heshima, na matumaini ya maisha bora kwa kila mmoja.
Makala hii inaangazia sio tu mafanikio haya ya kihistoria,bali pia jinsi mfuko huu unavyothibitisha kuwa hifadhi ya jamii si hifadhi ya fedha tu, bali ni uwekezaji katika utu wa binadamu na maendeleo endelevu.
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umejidhihirisha kama mhimili wa maisha bora kwa wastaafu, hususani kupitia hatua yake ya kulipa mafao ya Shilingi bilioni 126 kwa miezi mitatu.
Hatua hii inaashiria umuhimu wa mfumo wa hifadhi ya jamii katika ngazi ya mtu binafsi, familia, na taifa kwa ujumla kwa hiyo ni nguzo muhimu kwa wastaafu ambao mara nyingi hukabiliana na changamoto za kifedha baada ya kustaafu.
Kupitia PSSSF, wastaafu wanapata mafao yanayowasaidia kukidhi mahitaji yao ya kila siku, kama vile chakula, huduma za afya, na elimu kwa watoto wao ambapo fedha hizo huchochea uwekezaji wa ndani, ikiwa ni pamoja na miradi midogo midogo inayosaidia kuongeza kipato.
Yessaya Mwakifulefule Meneja uhusiano na elimu kwa wanachama PSSSF katika taarifa ya hivi karibuni alisema mfuko huo una malipo ya aina 2 kuna malipo 2 % yanayolipwa moja na PSSSF, na pia kuna malipo ya 7% yanayolipwa na serikali.
Kwenye 2% kuna wastaafu ambao wamestaafu kwa mujibu wa sheria kuanzia kipindi mwezi julai hadi Disemba mwaka huu 2024 wameingia kwenye sheria mpya ilioboreshwa bungeni jumla ya wastaafu 983 wamelipwa mafao yao.

“Wastaafu wa 7% wamelipwa jumla yao 1,984 kwa hiyo katika kipengele hicho jumla ya wastaafu 2,967 kiasi cha silingi Bilioni 23 zimelipwa kwa wastaafu hao” alisema Mwakifulefule.
Pamoja na hao kuna wale waliokuwa wakilalamikia mapunjo ambao walilipwa kwa mujibu wa sheria ya kikokotoo iliokuwepo tangu mwaka 2022, ambao walilipwa kwa viwango ambavyo havikuwaridhisha kwa hiyo baada ya maboresho walilipwa mapunjo yao.
“Kati yao waliokuwa wanalipwa na sisi PSSSF ni wastaafu 3,364 ambao malipo yao ni 2% lakini wale wa 7% wa serikalini ni 9,803 kwa hiyo katika kundi hili kulikuwa na jumla ya wastaafu 13,167 ambao jumla yao walilipwa Bil. 103 kwa hiyo kwa ujumla tumeweza kulipa jumla ya Bil. 126 kwa wastaafu wa aina hizo mbili “alisema.
Alisema kuwa malipo hayo yanaonesha jinsi gani mfuko huo ulivyoimarika kulipa mafao ya wastaafu bila kutetereka, ambapo kwa sasa mfuko huo umeenea nchi nzima ukiwa na wanachama wa aina zote ikiwemo wanachama wa serikali kuu, serikali za mitaa, waalimu na maafisa tarafa na wengine.
Alisema kuwa mfuko huo unalenga kuboresha ya wanachama na wastaafu wake ambapo ili uwe mnufaika kama mstaafu tarehe ya kustaafu ni lazima mfuko uwe umepokea michango yote ya mwanachama.
Kwa mujibu wa Ziada Obedy Mahava Meneja PSSSF kanda ya Mashariki alisema mwitikio ni mzuri kwa wanachama wake katika kanda zote 11, hivyo ni wajibu wa kila mwanachama kuujua vizuri mfumo wa mfuko huo ili kunufaika na mafao.
Alisema kuwa Mfuko wa Jamii PSSSF umejikita pia katika utoaji wa elimu kuhusu PSSSF kidigitali kuhakikisha waajiri wote wanaufahamu na kujua namna ya kuutumia ambapo elimu hiyo pia iliwafikia wanachama kuelewa mfumo huo kuepusha changamoto ya ucheleweshaji wa mafao.
“Kwa ngazi ya kanda malalamiko yamepungua sana niseme kiujumla yameisha kwa sababu tumelipa mafao yote ya muda mrefu na muda mfupi, mara nyingi malalamiko yako kwenye maslahi ukichelewesha malipo kwa mwanachama umegusa maisha yake umemgusa yeye binafsi pamoja na familia au ndugu kwa sababu huwezi jua anategemewa na nani” alisema Meneja Mahava.
Hata hivyo wastaafu wengi wanapostaafu wanategemea familia zao na jamii kwa msaada kwa hiyo Malipo hayo yatapunguza malalamiko kwa wastaafu, na hivyo kuongeza matumaini furaha na amani.
Wastaafu wengi wanakosa huduma bora za afya na elimu baada ya kustaafu, lakini malipo haya yanaweza kuwasaidia kugharamia matibabu, kujihusisha na shughuli za kijamii, au hata kusaidia watoto wao kupata elimu bora.
Bilioni 126 zilizolipwa kwa wastaafu si tu fedha, bali ni kiashiria cha mabadiliko katika maisha ya wastaafu na kuboresha maisha ya wastaafu na kuongeza tija kwa jamii nzima ambayo pia kuwa mfano mzuri wa hatua za maendeleo katika huduma za kijamii, na kuongeza “kicheko” cha matumaini kwa wote .
MWISHO.