Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro na Mipango ya Kufikia Malengo ya Taifa

Na Angela Kibwana, Morogoro

Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro imejipanga kuimarisha utawala wa sheria nchini kupitia maadhimisho ya Wiki ya Sheria 2025, ambayo yatakuwa na lengo kuu la kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa haki, usawa na utawala bora.

Katika mkutano uliofanyika na waandishi wa habari, Kaimu Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Mhe. Stephen Murimi Magoiga, alifafanua mipango ya maadhimisho hayo, akisisitiza kwamba Mahakama ina jukumu kubwa katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro Mheshimiwa Murimi amesema katika maadhimisho ya Wiki ya Sheria 2025, Mahakama ina Nafasi Kubwa katika Kufikia Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.

Maadhimisho hayo yatakayoanza Januari 25 hadi Februari 1, mwaka huu 2025, yatashirikisha wadau mbalimbali, wakiwemo viongozi wa serikali, taasisi za kisheria, na wananchi, katika kujenga imani na ufahamu zaidi kuhusu mfumo wa sheria na haki nchini.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro Mheshimiwa Stephen Murimi Magoiga akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya wiki ya sheria 2025

Akifafanua zaidi kuhusu maadhimisho ya mwaka huu, Mhe. Murimi alisema kuwa uzinduzi wa Wiki ya Sheria kwa Kanda ya Morogoro utaanza rasmi Januari 25, mwaka huu 2025.

Katika hafla hiyo, matembezi ya maandamano yatakayohusisha washiriki wasiopungua 1,000, yataanzia katika viwanja vya Mahakama IJC Morogoro, na yataelekea kwenye stendi ya zamani ya mabasi.

Maadhimisho haya yatahudhuriwa na wadau mbalimbali, wakiwemo watumishi wa Mahakama, Jogging Club 22, vijana wa Scout, Jeshi la Polisi, Jeshi la Zima Moto, wasanii, wanavyuo, na wananchi kwa ujumla.

Kwa mwaka huu, Kanda ya Morogoro inatarajia kutoa elimu kupitia maonesho ya kisheria ambayo yatafanyika katika mabanda yaliyopangwa katika maeneo mbalimbali.

Katika hotuba yake, Mhe. Murimi alieleza kuwa kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Tanzania ya 2050: Nafasi ya Taasisi Zinazosimamia Haki Madai katika Kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.” Alisema kauli mbiu hii inaonyesha umuhimu wa ushirikiano wa pamoja kati ya taasisi za kisheria, serikali, na wananchi katika kuhakikisha haki inapatikana kwa wote.

Baadhi ya watumishi wa mahakama kuu kanda ya morogoro na waandishi wa habari wakimsikiliza Kaimu Jaji Mfawidhi Stephen Murimi Magoiga

Alisisitiza kuwa Mahakama ina jukumu muhimu katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo, ambapo Tanzania inatarajiwa kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi wa kati na maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2050.

“Dira hii imejengwa juu ya nguzo kuu tatu ambazo uchumi imara, Jumuishi na shindani, nguzo ya pili ni uwezo wa watu na maendeleo ya jamii na nguzo ya tatu ni uhifadhi wa mazingira na uhimilivu wa mabadiliko ya tabia nchi” alisema Kaimu Jaji mfawidhi Murimi.

Katika maadhimisho ya wiki ya sheria Mahakama kuu kanda ya Morogoro imedhamiria kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa nguvu ya pamoja ya taasisi zote zinazosimamia haki madai katika kuleta tija na ufanisi kuwezesha kufikia malengo yaliowekwa kitaifa.

Pia alizungumzia umuhimu wa kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi, akieleza kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro imeanzisha kituo cha utoaji huduma za elimu ya kisheria katika viwanja vya Stendi ya Treni ya Mwendokasi ya Jakaya Mrisho Kikwete (SGR) ambapo kituo hiki kitakuwa na lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi na kutoa ufahamu kuhusu haki zao za kisheria, huku wakielewa na kushirikiana na wadau wa sekta ya sheria

Aidha, alisisitiza kuwa upatikanaji wa haki ni mchakato wa kushirikiana kwa karibu na wadau wa haki jinai na madai, na kwamba Mahakama itakuwa mstari wa mbele katika kutekeleza nguzo za Dira ya Taifa ya Maendeleo, ikiwa ni pamoja na usimamizi wa haki kwa wakati na bila ubaguzi.

Katika hatua nyingine, Mhe. Murimi alizungumzia umuhimu wa Mahakama Kuu katika kufikia malengo ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kuhakikisha mifumo ya sheria inafanya kazi kwa ufanisi.

Alisisitiza kuwa Mahakama ina jukumu muhimu katika kufanikisha utawala bora, amani, usalama, na ustahimilivu kwa kuamua mashauri kwa haki na kwa kufuata misingi ya kisheria. Alihimiza jamii kuendelea kushirikiana na taasisi zinazohusika katika utekelezaji wa haki, ikiwemo kutumia njia mbadala za utatuzi wa migogoro.

Mhe. Murimi pia alitangaza kwamba maadhimisho ya Siku ya Sheria Kitaifa yatafanyika Februari 3, mwaka 2025, katika viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma, ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi.

Alieleza kuwa kilele cha maadhimisho hayo, kilichopangwa kufanyika Februari 1, mwaka 2025, kitakuwa na muktadha wa kuzungumzia nafasi ya taasisi zinazosimamia haki katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.

Mhe. Murimi alimalizia kwa kusema kuwa ili kufikia maendeleo endelevu, ni muhimu kwamba mifumo ya sheria ifanye kazi kwa ufanisi na kuhakikisha haki inapatikana kwa kila mtu bila ubaguzi.

Alisisitiza kuwa ushirikiano wa pamoja kati ya taasisi za kisheria na wadau wengine utasaidia katika kutimiza malengo ya maendeleo endelevu na kuhakikisha utawala bora, amani, na usalama wa kijamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *