Askofu Mkuu  Kinyaiya azindua nyumba ya sala na Mafungo ya mapadre Wakarmeli Dodoma

Na Angela Kibwana, Dodoma.

Mhasham Askofu Mkuu Beatus Michael Kinyaiya wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma amezindua rasmi nyumba ya sala na mafungo ya mapadre wa Shirika la Karmeli ambayo itawawezesha wanakanisa kwa ujumla kufanya hija ya maisha ya kiroho kwa kufanya tafakari ya kina ili kujitakatifuza kiroho.

Askofu Mkuu Kinyaiya amewashukuru wamisionari wa Shirika la Wakarmeli Provinsi ya Tanzania kwa kueneza utume wao katika maeneo ya majimbo katoliki nchini ili kurahisisha huduma za kiroho kwa waamini na watu wenye mapenzi mema.

Askofu Mkuu Kinyaiya amesema hayo katika mahubiri wakati wa uzinduzi wa nyumba ya sala ya shirika la Wakarmeli iliyopo Chamwino Jimbo Kuu Katoliki Dodoma, akisema kuwa wamisionari hao wamekuwa ni chachu ya kukoleza imani kwa waamini wakatoliki.

Aidha amesema kuwa kiubinadamu kila mmoja akijichunguza kwa undani atagundua kwamba ni mkoma kwa namna fulani ambapo hali ya ukoma huo inadhihirishwa hasa mtu anapotenda dhambi anakuwa mkoma kiroho hususani anaposhindwa kufanya kitubio kwa maungamo.

“Kila tunapotenda dhambi tunakuwa wakoma kiroho,na mbaya zaidi kama unamkosea Mungu halafu hufanyi lolote yaani huhangaiki kutubu kutafuta msaada kumrudia Mungu inakuwa ni kama ukoma unavyokaa taratibu mpaka inafika mahali hali inakuwa mbaya” alisema askofu Kinyaiya.

Aidha askofu Mkuu Kinyaiya amesema kuwa baadhi ya watu katika maisha, wanapopata dhoruba na changamoto za maisha wanafikia hatua ya kujidhuru kutokana na kujenga mazoea ya kuwa na mlundikano wa vitu bila kumpa Mungu nafasi ya kutenda kadiri ya maoenzi yake.

Amefafanua kwamba baadhi ya watu katika maisha ya hapa duniani, wakipata changamoto kubwa wanaweza wa kuachana nayo na kutafuta mbinu nyingine za kutoka katika shida zao, lakini wengine wakipata shida wanaishia kujiua kwa sababu na kukosa msaada wa kiushauri.

Katika Muktadha huo askofu Mkuu Kinyaiya amebainisha kuwa kituo hicho cha sala moja ya kazi yake  ni kuwasaidia waamini wasije wakafika mahali kwa kukosa msaada au kukosa mtu wa kuwashauri na kuwasaidia kiroho ikiwa ni pamoja na kupata sakramenti ya maungamo na huduma nyingine za kiroho.

“Ndio maana nasema nashukuru Mungu shirika la Karmeli limekuja kwetu, na nina amini itatusaidia sisi wote mlio majirani na watu wote walio mbali ili daima ukoma wa kiroho uwe unasafishika kutusaidia kukutana na kristo mara nyingi zaidi ili hali zetu za kiroho ziwe nzuri, ” alisema askofu mkuu Kinyaiya.

Amesema kituo hicho cha sala ni sehemu ya kufanya  tafakari ya maisha ya kiroho kwa watu wote mapadre mahalia, watawa wa kike na wa kiume, makundi ya familia ikiwemo makundi ya kikristo kama vile wanakwaya , na makundi mengine ya vyama vya kitume hasa wanawake wakatoliki [WAWATA] na Uwaka.

Sambamba na hayo amewakumbusha waamini kujenga tabia ya kumshukuru Mungu kwa mema na Baraka nyingi anazowajalia katika maisha yao ya kila siku badala ya kuwa na mitazamo ya kuona kwamba kila walichojaliwa ni haki yao bila kumpa Mungu sifa na shukrani.

Mwishoni nAmewakumbusha wananchi wa maeneo jirani wanaoishi kando kando ya kituo hicho cha sala kusaidia utulivu wa eneo hilo liwe la sala kama ilivyokusudiwa ili watu wote watakaofika mahali hapo kwa ajili ya kuzimbea familia zao na nia nyinginezo wajichotee neema na Baraka kutoka kwa Mungu mwenyezi

“Nimalize kwa kuwaomba wanakijiji hapa jirani kutambua kwamba hili ni eneo la sala niwaombe msaidie mazingira ya hapa yawe ya sala, naomba nyumba sio nyingi lakini watakapoanza kujenga waambieni na wengine eneo hili liwe eneo la ukimya ,ukifungulia muziki wa bongo fleva kwa sauti ya juu utakuwa umetunyanyasa sote”alisisitiza.

Kwa upande wake Padre Elius Modest Malale Mkuu wa Shirika la Karmeli Provinsi ya Tanzania, amewashuru watangulizi wake wakuu wa shirika awamu zilizopita akianza na Padre Silvester Msemwa ambaye aliabuni wazo la kufanya utume katika Jimbo kuu Katoliki Dodoma,ambapo matunda yameanza kuonekana

Lakini pia Padre Malale alimshukuru na kumpongeza mtangulizi wake katika uongozi Padre Praven Frank ambaye alianzisha wazo la kujenga nyumba ya sala ambapo kukamilika kwake kumetokana na juhudi za watu mbalimbali kutoka katika parokia ambazo mapadre wa shirika hilo wanafanya kazi katika majimbo ya Mbeya, Dodoma, Songea, Dar es salaam na Morogoro waliojitolea kwa michango kukamilisha ujenzi wa nyumba hiyo.

Amewashukuru pia wafadhili na wadau mbalimbali waliofanikisha upatikanaji wa fedha kukamilisha uwepo wa kituo hicho cha sala na mafungo ili waamini waendelee kukua kiroho na kimwili.

Mkuu huyo wa Shirika amesema kuwa baada ya kuzinduliwa kwa kituo hicho cha sala na mafungo wanatarajia kuanza rasmi huduma ya semina kadiri walivyojipangia kwa kuzingatia miongozo ya Mhashamu askofu Mkuu Beatus Kinyaiya ili kuhakikisha huduma za kichungaji zinafanyika kwa uaminifu.

Ndani ya jengo hilo la kisasa kuna huduma mbalimbali hasa ukumbi wa kupokelea wageni , Kanisa dogo lenye sakrestia yake kwa sababu ni nyumba ya sala lazima kuzingatia hilo, kuna kanisa la kuabudia, vyumba vya kulala 30 vyote ni selfcontained, vyumba vya ziada vya wageni, ofisi mbalimbali, kumbi za mikutano,chumba cha maongezi ya binafsi na  bwalo la kulia chakula na huduma nyingine kulingana na mahitaji ya jengo.

Mwisho. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *