Mkuu wa wilaya ya Same aagiza kukamatwa kwa wahusika waliowapa ujauzito wanafunzi wanne wa shule za msingi na sekondari.

Na Angela Kibwana, Same.

Mkuu wa Wilaya ya Same,Kasilda Mgeni ameliagiza Jeshi la Polisi wilayani humo kuwasaka wahusika waliowapatia ujauzito wanafunzi wanne wa shule za msingi na sekondari baada ya kuwasababishia kosa la kukatiza haki yao msingi ya msingi ya elimu.

Mheshimimiwa Mgeni amesema hayo Kufuatia taarifa za ujauzito kwa wanafunzi hao wa shule tofauti za msingi na sekondari katika kata za Kalemawe na Bendera,

Na kutoa agizo la kukamatwa kwa wahusika wa matukio hayo haraka iwezekanavyo ili kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Katika ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi wilayani humo amewakumbusha wazazi na walezi kutambua umuhimu wa elimu ambayo ni haki msingi ya kila mtoto kuhakikisha wanatimiza ndoto zao kupitia elimu.

Aidha Mgeni amesema kuwa wapo wazazi wanaofanya ukatili kwa watoto wao kumalizana kindugu na wahusika wanaosababisha ujauzito kwa wanafunzi wa kike kushindwa kufikia malengo ya kupata elimu bora kwa sababu vitendo hivyo vinaharibu ndoto za watoto wa kike na juhudi za serikali kwa ujumla.

Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania imeweka mikakati ya kuboresha mifumo ya elimu nchini ili kutekeleza dhamira ya serikali inatekelezwa kwa malengo mahususi hasa kuwezesha wasichana wengi waliopo shuleni kutimiza malengo ya kupata elimu bora ili kujikomboa kifikra na kielimu.

“Mtoto wako amepata ujauzito amekatiza ndoto zake za kupata elimu, mzazi unapewa kitu kidogo na mtu aliyempa mimba mtoto wako mnakubaliana na mnamalizana na mnawafundisha hawa watoto wanaopata mimba wakipelekwa kutoa ushahidi wanasema simjui aliyenipa mimba,sababu mzazi umeshapewa hongo, hili jambo silitaki kwenye wilaya yangu” alisema Mhe. Mgeni.

Wazazi wote wanne ambao watoto wao walipata ujauzito na kumalizana kienyeji wanapaswa kukamatwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria kwa sababu wametenda kosa la kuwanyima watoto haki ya kusoma, adhabu ya mbakaji anapaswa kuchukuliwa hatua kifungo ni miaka 30.

“Mmekaa na wabakaji sasa ninyi ndio mtakaa jela badala yake sisi wanawake tunakaa na watoto tumboni miezi 9 iweje mtoto apate mimba kirahisi halafu tunanyamaza? Haiwezekani kwa sababu wabakaji wapo na wazazi mmeamua kuwaficha sasa tutaanza na ninyi, mtupe ushahidi vinginevyo mtuletee wabakaji wa watoto hawa, ninyi mtakuwa salama lakini kama ulipokea kitu kidogo wewe na huyo mbakaji kumbuka sheria ni msumemo itakata pande zote

Alisema kuwa serikali imejikita kuboresha mazingira rafiki ya elimu kwa wanafunzi wote, hasa wa kike, hivyo maboresho ya serikali katika mfumo wa elimu yanahitaji msaada wa jamii hivyo vitendo vya ubakaji na ukatili kwa wanafunzi havikubaliki, vinaharibu ndoto za watoto wa kike kufikia ndoto zao

Wananchi walioshiriki mkutano huo walionesha kuridhishwa na hatua za haraka zilizochukuliwa na Mhe. Kasilda, huku wakiahidi kushirikiana na serikali kwa kutoa taarifa za wahusika wa vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanafunzi.

Kwa upande wao, walimu wakuu wa shule hizo wameeleza kuwa wamesikitishwa na taarifa za kukatishwa masomo kwa wanafunzi hao kukatishwa ndoto zao, hivyo wameahidi kutoa ushirikiano kwa serikali  kufanikisha mipango yake ya kumkomboa mtoto wa kike kupitia elimu

Aidha walimu hao wamebainisha kuwa changamoto ya kutowatia mbaroni wahusika wa vitendo hivyo ni ushirikiano mdogo kutoka kwa wazazi wa wahanga husika, ambao mara nyingi huficha ukweli na kuweka vikwazo katika upatikanaji wa ushahidi wa utakaowezesha upatikanaji wa haki kisheria.

Sheria ya mtoto ya mwaka 2009 nchini Tanzania inalinda haki za watoto ikiwemo haki ya kupata elimu, afya, na ulinzi dhidi ya aina zote za unyanyasaji wa kisaikolojia au kimwili.

Mimba za utotoni mara nyingi huhusishwa na ukiukwaji wa haki za wasichana, ibara ya 5 inaeleza haki za watoto ikiwemo haki ya elimu, huku ibara ya 13 ikihusu ulinzi dhidi ya unyanyasaji jambo linalochangia mimba za mapema kwa wasichana.

Kitaifa kiwango cha mimba za utotoni umri wa miaka 10-19 kimepungua kutoka asilimia 27 hadi kufikia asilimia 22 kwa mujibu wa utafiti wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya Malaria Tanzania [TDHS] ya mwaka 2015/2016 na 2022.

Sababu zinazochangia uwepo wa tatizo hili ni pamoja na ukosefu wa taarifa sahihi zinazohusiana na masuala ya afya ya uzazi, unyanyasaji wa kijinsia ndoa za mapema na ushirikiano mdogo kutoka kwa wazazi.

Mwisho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *