Mahakama yajizatiti kusimamia Haki kwa Maendeleo Endelevu ifikapo 2050

Na Angela Kibwana, Morogoro.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu kanda ya Morogoro Stephen Murimi Magoiga amesema ifikapo mwaka 2050 Tanzania inatarajiwa kuwa kati ya nchi zenye uchumi wa kati ngazi ya juu au zaidi shabaha kuu katika mpango huo umejikita katika dhima ya kuwa taifa jumuishi lenye ustawi, haki linalojitegemea

 Amesema hayo katika maadhimisho ya siku ya sheria nchini iliyokwenda sambamba na uzinduzi wa mwaka mpya wa mahakama  iliyofanyika katika kituo jumuishi cha Utoaji haki IJC Mkoani Morogoro kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wa haki mada ikiwemo  viongozi wa dini na watu mbalimbali.

Aidha amesema kuwa ili taifa liwe na maendeleo endelevu ni lazima misingi ya haki isimamiwe kwa uaminifu na haki, hivyo ikiwa mihimili inayohusika na usimamizi wa haki ikishindwa kusimamia kwa uaminifu, haki za watu zitaminywa na taifa halitafikia malengo yaliowekwa kwa sababu asiye na haki huinua migogoro dhidi ya mwenye haki.

Katika hatua za maendeleo ya taifa, haki madai ni uti wa mgongo katika kufanikisha mambo kadhaa katika dira ya maendeleo yaliowekwa hasa kuvutia mazingira mazuri ya uwekezaji kwa kuweka sheria rafiki na rahisi kuwavutia wawekezaji kuwekeza hapa nchini, kuhakikisha uko ulinzi na usalama wa kisheria katika kulinda haki za uwekezaji na uzalishaji katika nchi.

Mpango mkakati wa mahakama zinaweka msingi wa mahakama kuhakikisha mahakama inasimamia upataikanaji wa haki kwa wote na kwa wakati ili kutekeleza malengo endelevu ya kitaifa.

Katika kusimamia hilo Mahakama za mwanzo zimefanikiwa kikamilifu hadi kufikia mwisho wa mwaka 2024 jumla ya mahakama 34 zilivuka mwaka bila kubakiza kesi yoyote ambayo haijasikilizwa kutolewa uamuzi, katika mahakama hizo ziko wilaya ambazo wanasimamia kesi kwenye mahakama zote za mwanzo zilizopo kwenye wilaya zao.

“Mahakama hizo ni wilaya ya Morogoro   Malinyi, na ulanga aidha wilaya ya kilombero walisaliwa na kesi 02 pekee, nitumie nafasi hii kuwapongeza waheshimiwa mahakimu wote wa mahakama za mwanzo, mahakimu wafawidhi wao, maafisa utumishi kwa kusimamia adhma hiyo kikamilifu muda ambao wananchi wangetumia kufuatilia mashauri yao mahakamani wameutumia kwa shughuli za uzalishaji kwa kuwa migogoro yao imetatuliwa” alisema Mh Magoiga.

Sambamba na hayo katika kutekeleza nguzo ya tatu ya mpango mkakati wa mahakama, Mahakama inatambua kuwa mafanikio ya jamii hayawezi kutokea kwa juhudi za upande mmoja tu bali mnyororo wa haki madai ni muunganiko  na ushirikiano wa mahakama na wadau wa haki madai.

Katika mahakama za kanda ya Morogoro wameendelea kuwa na ushirikiano mzuri na wadau wa haki madai na hivyo kuongeza ufanisi katika jukumu msingi la utekelezaji  wa utoaji haki, ambapo hadi kufikia disemba 31 mwaka 2024 mahakama kuu kanda ya Morogoro ilikuwa imepokea mashauri 803,kwa mwaka wa 2024

Amefafanua kuwa idadi hiyo inajumuisha mashauri 443 yaliobaki Desemba 2023 na kufanya jumla ya mashauri 1,246 ambapo mashauri yalioamriwa hadi kufikia Disemba 24 ni 948, yaliosalia ikiwa ni 298.

Amesema kati ya mashauri yaliofunguliwa mwaka 2024 mashauri ya baadae ni sawa na 31% ya mashauri yote, ambapo katika aina ya madai husika mashauri ya ardhi ni 41% ya mashauri yote ya madai yaliofunguliwa.

Sambamba na hayo amashauri mengine ya madai ni pamoja na madai ya kawaida, rufaa za mashauri ya ndoa na talaka maombi madogo ya gharama na utekelezaji wa mashauri mengine, kuna umuhimu wa kueleza taarifa kwa takwimu ili kuona juhudi za mahakama katika utoaji haki.

“Mahakama ya hakimu mkazi imepokea mashauri 59 ya madai na kusikiliza mashauri 45 na kubaki mashauri 14, mashauri  yaliomalizika ni sawa 76% ya mashauri hayo , mahakama za wilaya zimepokea jumla ya mashauri  958 na kusikiliza mashauri 793 sawa na 83% ya mashauri yote yalioendelea kwa mwaka 2024 na mashauri yaliosalia ni 163” alisema.

Hata hivyo mahakama za mwanzo kwa 2024 zilikuwa na mashauri 6,109 ambapo mahakama hizo zilifanikiwa kusikiliza mashauri 5,948 na kubakiza mashauri 161 mashauri yaliomalizwa ni sawa na 97% ya mashauri yote, hivyo Mahakama kuu kanda ya Morogoro imeahidi kufanya vizuri zaidi kwa mwaka 2025.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima ametoa ombi kwa mahakama kuendelea kutoa elimu kwa jamii kutokana idadi kubwa ya watu kupoteza haki zao kwa sababu ya kutojua sheria za kutatua migogoro ili kupata haki zao

Amesema kuwa ndani ya jamii wapo wajane na makundi mengine wanaopoteza haki zao kwa sababu ya kukosekana kwa ufahamu wa masuala ya sheria  ili kila mmoja aweze kupata haki zake za msingi,watu wanapofahamu sheria ni rahisi kutetea haki zao ili wawe bora zaidi

“Naomba niwahakikishie kwamba ofisi yangu itakuwa mstari wa mbele kwa mambo yoyote ambayo mahakama ya tanzania inataka kufanya katika kukuza uelewa wa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya msingi ya kisheria hili ni jukumu na wajibu kwa sisi wote kuhakikisha kwamba watanzania hawapotezi haki zao za msingi kwa sababu ya kutokujua haki za kisheria”

Ikukmbukwe kwamba pale ambapo hakuna haki hakuna amani, na pasipo na amani hakuna ustawi wa binadamu, Tanzania ni mfano mzuri wa nchi yenye amani kwa sababu inaendesha mambo yake kwa kuzingatia haki kupitia mahakama ya Tanzania ambayo ndio muhimili pekee wa kutoa maamuzi.

Mwisho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *