Askofu Msimbe ahimiza waamini kuviwezesha vyombo vya habari vya Kanisa kukuza Uinjilishaji.

Na Angela Kibwana, Morogoro

Askofu wa Jimbo katoliki Morogoro Mhasham Lazarus Msimbe Sds amepongeza uwepo wa vyombo vya habari za Kanisa katoliki ambavyo vimeongeza chachu ya kuimarisha imani kwa waamini kupitia habari za uinjilishaji na vipindi vya kiimani.

Askofu Msimbe amesema hayo katika mahijiano maalum na mwandishi wetu akisema kwamba uwepo wa vyombo vya habari vya Kanisa vinamsaidia kujiandaa vizuri katika mahubiri yake ili waamini waweze kulishwa neno la Mungu kwa njia ya mahubiri.

Aidha amesema kuwa kwa njia ya vyombo vya habari ujumbe wa neno la Mungu unafika katika maeneo mengi ambapo viongozi wa dini si rahisi kufikia waamini wote kutokana na miundombinu ya kijiografia hivyo ameomba vyombo vya habari vya Kanisa kutafuta habari zinazogusa watu waishio pembezoni.

Askofu Msimbe amesema kuwa vyombo vya habari vinapaswa kusimamiwa kwa uaminifu kuendelezwa na kutunzwa ili kuhakikisha vinasaidia kukuza uinjilishaji wa habari,na ujumbe wa neno la Mungu ili kuimarisha imani kwa waamini.

“Ninamshukuru Mungu kwa uwepo wa Vyombo vya Habari  vya Kanisa kwa jimbo la Morogoro ninapata mrejesho mzuri kutoka kwa waamini ambao wanafuatilia vipindi na habari mbalimbali zinazolihusu Kanisa hivyo ni msaada mkubwa kwa imani za wakristo” amesema askofu Msimbe.

Amesema uwepo wa Radio Ukweli ya Jimbo la Morogoro, Radio Maria Tanzania, Radio Tumaini, gazeti Kiongozi na Jugo Media, vyombo hivi vimesaidia waamini kupata habari za matukio mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kuhusu Imani na Katekesi za mafundisho mbalimbali zinasaidia waamini kupata habari za kanisa kwa urahisi zaidi.

Ameongeza kuwa kwa kutambua umuhimu wa vyombo vya habari mara kwa mara katika ziara zake za kichungaji huambatana na vyombo vya habari vya Kanisa ili kuwezesha ujumbe wa neno la Mungu kuwafikia waamini wa haraka zaidi hasa waishio vijijini.

Amesema kuwa ni fursa nzuri kupeleka ujumbe wa neno la Mungu kwa njia ya vyombo vya habari,anasema awali alipata hofu kujua waandishi wa habari watapeleka ujumbe gani kwa watu endapo kama watarekodi kila kitu anachozungumza kwa njia ya mahubiri, hivyo ilimsaidia kujiandaa vizuri na kutetea chochote ambacho kitatangazwa na vyombo vya habari.

“Kila ninapoongea najiandaa vizuri zaidi niweze kuongea ujumbe ambao utawafaa waamini na watu wote kwa ujumla,na kilichonipa nguvu ni kwamba Kristu mwenyewe alituambia tupeleke habari njema ulimwenguni kote, mimi kama mimi askofu wa jimbo siwezi kwenda ulimwenguni kote, ni vyombo vya habari ndivyo vinavyonisaidia kupeleka ujumbe wa habari njema ulimwenguni, ndio maana navutiwa na uwepo wa vyombo vya habari”

Ametumia fursa hiyo kuwahimiza waamini na watu wenye mapenzi mema kuchangia na kuviwezesha vyombo vya habari vya Kanisa ili viweze kujiendesha na kufanya utume wake kikamilifu.

Idadi ya waamini wakatoliki kwa sasa Jimboni Morogoro ni 912,000 waamini hawa wengi wao wanakosa fursa ya kumuona askofu mara kwa mara, ambapo kupitia vyombo vya habari vya Kanisa wanapata ujumbe wa neno la Mungu kwa njia ya Redio na magazeti ya Kanisa Katoliki.

Sambamba na hayo askofu Msimbe amesema kuwa vyombo vya habari kwa ujumla vina mchango mkubwa kuhabarisha masuala mbalimbali ya kijamii, hususani kuibua matukio ya ukatili ikiwemo kupata ujumbe wa viongozi wanaokemea vitendo hivyo ili kudumisha maadili na amani kwa ujumla.

Kufuatia vitendo vya matukio ya ukatili, serikali imekuwa ikihimiza viongoyi wa dini kutumia nyumba za ibada kukemea vitendo hivyo,sambamba na kuwahimiza waamini kuishi maadili mema yatakayowezesha taifa kuwa na utulivu wa Amani kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *