Na Angela Kibwana, Morogoro.
Askofu wa Jimbo Katoliki Morogoro mhashamu Lazarus Msimbe SDS ameitaka Jamii kuepuka vitendo vya unyanyasaji dhidi ya watu wenye ulemavu kwa kuwaonyesha upendo kutokana na wengi wao kutengwa katika jamii wanazoishi.
Askofu Msimbe alitoa kauli hiyo wakati wa mahubiri kwenye ibada ya Misa Takatifu ya kuweka ahadi za Kwanza kwa watawa sita wa shirika la Bikira Maria Malkia wa Amani wanaojihusisha na malezi ya watoto wenye ulemavu wa viungo na akili waliopo kituo cha Amani kinachomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimboni humo.
Aidha katika mahubiri yake askofu Msimbe alisema kuwa kuna watu ndani ya jamii wanaofanya ukatili dhidi ya watoto wenye ulemavu ambapo baadhi ya wazazi wanapozaa mtoto mwenye ulemavu wanawaangamiza kwa kupoteza maisha yao ikiwemo kunyimwa haki ya malezi bora kama wanavyohudumiwa watoto wengine.
Alisema kuwa kila mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ana wajibu wa kutetea uhai wa watu wengine kuhakikisha uwepo wa usawa katika katika makuzi ya maisha ya kawaida hadi umauti wa kawaida unapomkuta mwanadamu kadiri ya mapenzi ya Mungu.
Hata hivyo askofu Msimbe aliongeza kuwa watu wenye ulemavu wanahaki ya kuishi, kupendwa, kulindwa,kutumikiwa, kutunzwa na kusikilizwa kama walivyo watu wengine,kwa kuwa kundi hili linahitaji faraja ya pekee ili kuonjeshwa upendo wa Mungu ili kufurahia maisha ya kijamii.

“Tunafahamu wazi kabisa wapo watu wengi ambao wakizaa watoto wenye ulemavu baadhi yao huwa wanawaangamiza,kama wasipowapoteza maisha yao basi hawawatunzi kama inavyotakiwa, wapo wengine wanawaficha ndani, watoto wenye ulemavu nao wana haki ya kuishi uhai wao unapaswa kutunzwa” alisema askofu Msimbe.
Sambamba na hayo askofu Msimbe ametoa mwaliko kwa waamini Jimboni humo pamoja na watu wenye mapenzi mema kuwaombea watawa hao ambao wametolea sadaka ya maisha yao kuwatunza watoto wenye ulemavu ili kuwapenda, kuwahudumia, kuwatumiakia na kuwasaidia katika mahitaji yao ya kimwili na kiroho.
Alisema kuwa majitoleo ya kutunza uhai wa watoto hao wenye ulemavu wa viungo na akili ni sawa na kumtunza Yesu mwenyewe kwa kuwa licha ya ulemavu wao, wanahitaji msaada wa karibu kwa kuwa nao pia wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Akizungumzia kuhusu karama ya shirika hilo la Bikira Maria Malkia wa Amani ambayo ni kutetea, kuwapenda na kuwasaidia watoto wenye ulemavu amesema ni karama inayochochea upendo na kutetea uhai kwa watoto wenye ulemavu ambao wengi wao wanatengwa na jamii ikiwa ni pamoja na kunyimwa haki zao msingi upande wa elimu na afya.
“Mkiwapenda na kuwatumikia watoto hawa vema kama inavyoakiwa hakika majina yenu yataandikwa mbinguni, ni chaguo zuri mlilochagua kwa sababu kutunza uhai wao ni sawa na kumlina Yesu Kristo” alisema askofu Msimbe.
Askofu Msimbe amesema kuwa kukosekana kwa upendo ndani ya jamii kuna sababisha uwepo wa vitendo vya ukatili,kutokana na baadhi yao kuishi kama mafarisayo kwa kuishi maisha ya kuzingatia zaidi sheria kuliko utu na ubinadamu kiasi cha kuwatesa watu kutokana na sheria zao bila kujali ubinadamu
Amefafanua kuwa sheria kuu ya upendo ndio sheria kuu inayojali ubinadamu ikidai kwamba binadamu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kuliko kitu kingine chochote, hivyo askofu Msimbe ameeleza kuwa sheria kama haimsaidii binadamu haina maana yoyote ni bora ifutwe.
Wakati huo huo amesema kuwa katika jamii wapo watu wengi ambao wanampinga Kristo kwa kutenda mambo maovu ndani ya jamii ambayo ni chukizo kwa Mungu, ikiwa ni pamoja na kuhatarisha uhai wa binadamu.
Amesema wapo watu ndani ya jamii wanaoendelea kumpinga Kristo kwa njia mbalimbali kwa mawazo, maneno, matendo,unafiki na kwa njia nyingine na sambamba na kutoona thamani ya watu wengine, hivyo ametoa rai kwa jamii kuona thamani ya watoto wenye ulemavu kuwapatia heshima wanazostahili.
Naye padri Beatus Sewando mwanzilishi wa shirika la Bikira Maria Malkia wa Amani na Mkurugenzi wa kituo cha kuhudumia watoto wenye ulemavu cha Amani ameiomba jamii kukiangalia kituo hicho kwani kwa sasa kina mahitaji mengi katika kuhudumia watoto hao
Hata hivyo ametoa wito mabinti wengi kujitokeza kujiunga na utawa wa shirika hilo ili kusaidia malezi ya watoto hao ambao wengi wao wamekuwa wakinyanyasika katika jamii kutokana na ulemavu wao walio nao.
Sambamba na hayo Pauline Faustine mmoja wa watawa hao 6 walioweka ahadi ya kwanza kwenye Shirika la Bikira Maria Malkia wa Amani kwenye malezi ya watoto hao amesema anajisikia fahari kuwa miongoni mwa watoa huduma kutetea uhai kwa watoto hao ambao ni mfano wa Kristu
Kituo cha kuhudumia watoto wenye ulemavu wa akili na viungo cha Amani Morogoro kilianzishwa mwaka 1992 na aliyekuwa askofu wa jimbo Katoliki la Morogoro hayati askofu Adriani Mkoba askofu wa kwanza mzalendo wa Jimbo Katoliki Morogoro kufuatia wazo la mmoja wa wazazi Bi Josephine Bakhita aliyekuwa na mtoto mwenye ulemavu wa viungo na akili
Mwaka 2007 lilianzishwa shirika la Mama Bikira Maria Malkia wa Amani na aliyekuwa askofu wa jimbo la Morogoro Theresphor Mkude lengo likiwa ni kuwatumia watawa wa shirika hilo katika malezi ya watoto hao.
Sera na sheria kuhusu watu wenye ulemavu zinalenga kuhakikisha haki zao zinalindwa na wanajumuishwa kikamilifu katika jami, hata hivyo, Mkataba wa kimataifa wa haki za Watu Wenye Ulemavu (2006) unalenga kulinda haki na heshima ya watu wenye ulemavu, kuhakikisha usawa na kutokomeza ubaguzi katika nyanja zote za maisha.
Watawa walioweka nadhiri ni Sr Yasinta Abineli, Sr Vaileth Kamage, Sr Secilia Mwasenga, Sr Paulina Michael, Sr Gladis Timanywa na Sr Martha Sanga, Hadi sasa Shirika la Bikira Maria Malkia wa Amani lina jumla ya watawa 14 ambao wameweka nadhiri kwa ajili ya kutetea na kuhudumia watoto wenye ulemavu wa viungo na akili katika kituo cha Amani Jimboni Morogoro.
Mwisho.