Na Angela Kibwana, Morogoro.
Askofu wa Jimbo Katoliki Morogoro Mhasham Lazarus Msimbe SDS amesema utafiti unaonesha kuwa tatizo la afya ya akili linaongezeko ambapo takwimu kuhusu tatizo hilo zinaonyesha kuwa ni tatizo linaloathiri idadi kubwa ya watu duniani kote
Askofu Msimbe amesema hayo katika mahubiri ya adhimisho la Misa takatifu ya utoaji wa daraja takatifu ya upadre kwa mapadri wapya 9 wa Shirika la wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Provinsi ya Tanzania iliyofanyika katika Kanisa la Hija la Mwili na Damu Kola Jimboni Morogoro
Askofu Msimbe amesema kuwa afya ya akili ni hali ya ustawi wa akili ambayo huwezesha watu kukabiliana na changamoto za maisha kutambua uwezo wao kujifunza vizuri na kufanya kazi vizuri kwa manufaa ya jamii,kinyume chake ni tatizo la afya ya akili.
Aidha amefafanua kuwa tatizo la afya ya akili hakuna binadamu yeyote anayeweza kulikubali kiurahisi hata wale wenye changamoto hizo zinazoonekana kwa nje imekuwa ni ngumu kulikubali kwa sababu ya mifumo ya kibinadamu
Kwa Mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) taarifa ya mwaka 2019 kati ya 20-30% ya watu Afrika wana magonjwa ya akili ambapo tatizo hilo linaendelea kuathiri maisha ya watu kwa sababu ya huduma duni za afya ya akili kutokana na nchi nyingi za Afrika kuwa na wataalamu wachache.
Changamoto za afya ya akili zinachangia 16% ya Magonjwa, ajali hasa kwa vijana wa miaka 10-14, kuhusu changamoto za afya ya akili zinaanza kwa vijana katika umri wa miaka 14 ambapo kesi hizo hazitambuliki na wala hazitibiwi kutokana na kukosekana kwa wataalam wa kutosha
Miongoni wa changamoto ni huduma duni za afya ya akili Kwa mfano, kuna wastani wa mtaalamu 1 wa afya ya akili kwa kila watu 500,000 katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ikilinganishwa na wastani wa kimataifa wa mtaalamu 1 kwa kila watu 10,000.
Aidha Mitazamo ya Jamii inaathiri huduma za magonjwa hayo kwa sababu magonjwa ya akili mara nyingi yanahusishwa na imani potofu au unyanyapaa, hali inayozuia watu wengi kutafuta msaada

Shirika la Afya Duniani linaonyesha kuwa takriban 2-3% ya Watanzania wanaugua magonjwa makubwa ya akili kama vile schizophrenia kimsingi hadi 20% ya watu wanaweza kuwa na dalili za matatizo ya akili kama vile msongo wa mawazo na wasiwasi
Kuna upungufu mkubwa wa wataalamu wa afya ya akili. Tanzania ina madaktari wachache wa magonjwa ya akili, na hospitali chache zinazopeana huduma maalum huduma nyingi za afya ya akili bado zinapatikana katika hospitali kuu kama Hospitali ya Taifa Muhimbili na Hospitali ya Rufaa ya Mirembe Jijini Dodoma.
Kwa vijana wa miaka 15-19 katika sababu kuu tatu zinazochangia vifo ni pamoja na kujinyonga kwa kundi la vijana hii ni kwa mujibu wa taarifa ya dunia ya tafiti ya afya Tanzania Bara katika ripoti yake ya mwaka 2017.
Kwa hiyo Kanisa pia linapaswa kuwasaidia vijana kuondokana na changamoto hizo kwa kuwakutanisha vijana mara kwa mara na kuwa na dirisha la wazi kwa vijana ili kuona kwamba Kanisani ni sehemu ya kukimbilia na kutoa changamoto zao.
Pamoja na hayo viongozi wa dini pia wanapaswa kupewa elimu ya kutosha ili kuwa na ujuzi wa kuwasikiliza vijana kwa ajili ya kufanya canseling, kuwaepusha vijana na matatizo ya afya ya akili kwa kuwa ni vijana ndio hazina ya Kanisa.
Kwa ujumla tatizo la afya ya akili ni kitendo cha ubongo kushindwa kufanya kazi yake vizuri kwa maana ya kushindwa kufanya maamuzi,ambayo ni dalili ya kwanza kutambua mtu mwenye matatizo ya afya ya akili hasa jinsi anavyofanya mambo yake,matendo na tabia zake namna avyotofautiana na watu wengine katika kutenda na kufikiri
Kidunia inakadiriwa karibu watu 800,000 wanajinyonga kwa mwaka kutokana na changamoto ya afya ya akili ambayo ni sawa na kifo 01 kila baada ya sekunde 40, ambapo 78% ya takwimu hizo zinatokea kwenye nchi zenye uchumi wa chini na kati ambayo chanzo chake ni huduma duni, mazingira na mitazamo hasi ya kijamii.

“Tatizo la afya ya akili huwezi kulikubali hata tukimwambia yeyote hapa kwamba una tatizo la afya ya akili tukupeleke Milembe hawezi kulikubali utakataa kwa nguvu zote hata mwendawazimu pia ukimwambia tukupeleke Milembe hawezi kukubali hata mkimfunga na kamba, kutokuelewa kwamba wewe una tatizo la afya ya akili hilo ni tatizo kubwa zaidi”
Amesema kuwa moja ya kazi aliyofanya Yesu Kristu hapa duniani ni kufundisha watu, kadhalika mapadri wapya wanapowafundisha watu maana yake wanarekebisha afya ya akili za watu zikae sawasawa, na mapadri pia wana wajibu huo wa kufundisha kamaYesu mwenyewe alivyofundisha, Injili ya Mathayo 28:16-20.
Sambamba na hayo askofu Msimbe amewahimiza mapadri hao wapya wafundishe waamini kwa maisha yao yanayoakisi mifano ya mizuri ya utu wema, wafundishe kwa njia ya Katekesi na mahubiri ili watu waweze kumjua Mungu wampende, wamtumikie na mwisho wafike kwake.
Kuhusu namna ya kuhubiri amewakumbusha pia mapadri hao kuhubiri vizuri kuwa na muda wa kutosha kufanya maandalizi ya tafakari ya neno la Mungu kwa sababu wapo baadhi ya mapadri jumamosi usiku wanatumia muda mfupi kuandaa mahubiri hali ambayo inasababisha kuhubiri watu au kuongea mafumbo baina yake na muumini fulani kwa sababu hajajiandaa.
“Tutaweza kuwaponya watu sisi mapadri kama tutahubiri vizuri kwa sababu watu wana mahangaiko mengi wanahitaji sisi mapadre tuwaponye kwa mafundisho na mahubiri katika nyumba za ibada” alisema askofu Msimbe.
Wakati huo huo askofu Msimbe amesema kuwa katika tafiti zake alizofanya hivi karibuni amegundua kwamba kuna waamini wengi wakatoliki ambao wanatabia ya kwenda kwenye madhehebu mengine kusikiliza neno la Mungu, licha ya wale wanaohama kabisa imani katoliki kwa sababu ya kuchotwa na mafundisho yalio nje ya kinyume cha ukatoliki.
Amewakumbusha mapadri kuepuka tabia ya kutengeneza mianya ya kuwasababisha waamini kutoka ndani ya Kanisa lao na kwenda kwa wachungaji wa madhehebu mengine kusikiliza neno la Mungu huko ni kuwakosea haki waamini haki yao msingi kulishwa neno la Mungu.
“Mapadre wapya nanyi wa zamani ni tusitengeneze nafasi kama hiyo kwa waamini wetu kwamba hawashibi neno la Mungu mpaka wasikilize mahubiri ya makanisa mengine? Huu ni wajibu wetu ambao inabidi tuutilie mkazo, vinginevyo tutakuwa tunawakosea haki waamini wetu pia tunashindwa kuutendea haki upadri wetu” amesema askofu Msimbe.
Amesema tafiti zinaonesha kuwa kwa sasa kuna mmomonyoko mkubwa wa maadili katika jamii ambapo ukweli huo unathibitishwa na matendo mabaya ya wizi,ujambazi, rushwa, ushoga,ulawiti, ubakaji na utoaji mimba ambayo ni matendo yalio kinyume na mpango wa Mungu.
Amewasisitiza mapadri wapya kulinda na kusimamia maadili katika utume wao kwa Kanisa,kwa sababu mtu yeyote anaposhindwa kuishi kimaadili katika jamii heshima yake inashuka hakuna mtu yeyote atakayeheshimu hivyo mapadri wana wajibu wa kurudisha heshima kwa kukemea maovu ili watu wapone madhaifu yao yanayotokana na dhambi
Askofu wa Msimbe SDS amesema maisha ya binadamu kwa nyakati za sasa yanatishiwa na mahangaiko ya aina kuu tatu, ambayo ni mahangaiko ya kimwili, kiakili na kimaadili, ambayo yanasababisha athari mbalimbali na kimwili na kiroho kwa waamini na Kanisa kwa ujumla.
Amewaomba mapadri hao 9 waweze kuwa wachungaji wema waweze kuwaponya watu kimwili katika magonjwa na mahangaiko yao mbalimbali, kuwaponya watu kiakili na kuponya watu kimaadili ili watu waweze kuishi kiadilifu na kuwa na uzima tele kama alioagiza Yesu Kristu.
Mwisho.