Askofu Msimbe ataka Mashirika ya Kitawa kuongeza wigo wa huduma za kiroho vijijini.

Na Angela Kibwana, Morogoro

Askofu wa Jimbo Katoliki Morogoro Mhasham Lazarus Msimbe Sds, amesema Jimbo Katoliki Morogoro kwa sasa lina jumla ya waamini wakatoliki 912,000 mapadre 102 wa Jimbo wanaofanya utume katika parokia 78 za Jimbo hilo na vigango vingine ambayo vinatarajiwa kuwa parokia teule kwa siku zijazo

Askofu Msimbe amesema hayo katika maahojiano maalum na gazeti hili kueleza maendeleo na mafanikio ya shughuli za kichungaji Jimboni humo, akisema kwamba Jimbo la Morogoro ni kubwa kijiografia ambapo wanafanya mkakati wa kuongeza wigo katika shughuli za kichungaji na kiroho kwa waamini

Aidha amesema kuwa kutokana na ugumu wa miuondombinu na kuzidiwa na majukumu ya shughuli za kichungaji hasa wakati wa kutoa sakramenti ya kipaimara, askofu Msimbe analazimika kuomba usaidizi kwa askofu mstaafu Telesphor Mkude wa Jimbo hilo pamoja na makamu wa Askofu padre Salvinus Kwembe

Hadi sasa Jimbo hili lina ukubwa wa eneo la Kilomita za mraba 43,380 ikiwa ni 16,755 square miles ambalo linaundwa na wilaya sita za kiserikali, katika Manispaa ya Morogoro ndipo yalipo makao makuu ya Askofu wa Jimbo Katoliki Morogoro katika eneo la Kilakala.

Amesema kuwa Jimbo la Morogoro lilianzishwa mwaka 1953, ni miongoni mwa majimbo ambayo yana mashirika mbalimba ya kitawa na kazi za kitume ambao wanafanya utume Jimboni humo ambao wamekuwa msaada kusaidia huduma za kiroho kwa waamini katika parokia mbalimbali za Jimbo hilo.

Hivi karibuni askofu Msimbe alizindua sala maalum ya kuliombea Jimbo hilo lililopo chini ya tunza ya Mamam Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili, ili kuwashirikisha waamini katika familia na jumuiya zao kuziombea changamoto zinazolikabili Jimbo hilo.

Kwa mara ya kwanza Askofu Lazarus Msimbe amefanya misa maalum ya Kijimbo kuliombea Jimbo hilo katika viwanja vya seminari ndogo ya Mtakatifu Petro Morogoro, iliyokwenda sambamba na harambee ya kuwachangia waseminari wakubwa waliopo katika seminari kuu hapa nchini.

“Tangu mwezi mei mwaka huu tulianza kusali na kuliombea Jimbo letu ambali linapitia changamoto za kiimani, uchumi na mengineyo, tumeona kwamba tumtangulize Mungu katika changamoto zetu,kwa sababu Bwana asipoijenga nyumba wajengao wanakesha bure” nikapanga kuwaita wanajimbo wote kukusanyika pamoja ili tusali pamoja tumwelekezee Mungu nia zetu binafsi na kumlilia kwa pamoja shida zinazolikabili Jimbo letu”amesema Askofu Msimbe.

Hata hivyo amesema kuwa kila mwaka kutakuwa na Misa maalum kuliombea jimbo pamoja na harambee ya kupata fedha ya ada na matumizi mengine kwa ajili ya waseminari 63 waliopo kwa sasa ambao wanasoma falsafa na teolojia, matumizi yao ikiwa ni zaidi ya Milioni 150, ambayo ni ngumu kumudu gharama hizo kutokana na changamoto za uchumi zinazolikabili Jimbo kwa muda mrefu.

Sambamba na hayo amewaomba waamini Jimboni humo kuwaombea mapadre mara kwa mara ambao wanapata mateso na maumivu kwa ajili ya kuwahudumia kiroho waamini, wanapaswa kupewa faraja hasa wanapokumbana na dhoruba katika utume wao

“Tusiwatumie mapadre vibaya kuna baadhi ya waamini wana tabia ya kutafuta faida binafsi kwa kutengeneza urafiki wa kinafiki na mapadre, acheni tabia hiyo padre ni mhudumu wa watu wote, usije ukampoteza kwa unafiki na kumchanganya kwa sababu nae ni binadamu ukimchanganya anaweza akachanganyikiwa, wenye tabia hiyo muache”

 “Jitahidini kuishi katika ukweli wa imani padre atakupenda kwa ukristo wako mzuri na wala sio kumpa zawadi kwa unafiki ili upendwe, tuwaombee kwa Mungu ili awatie nguvu kuwaimarisha na kupata moyo wa kujitoa zaidi katika huduma zao za kiroho”

Wakati huo huo askofu Msimbe amewaomba mapadre wa mashirika ya Kitawa, kazi za kitume na kimisionari kujitoa kwa dhati kustawisha huduma ya kiroho kwa waamini waishio pembezoni ambao wanakosa fursa ya kupata misa Mara kwa mara kutoka kwa mapadre, kwa sababu vigango vingi vinahudumiwa na makatekesta

Amesema Vigango vingi Jimboni Morogoro vinakosa hadhi ya kuwa parokia teule kutokana na uhaba wa mapadre na miundombinu migumu ya kuwafikia waamini waishio pembezoni kutokana na ukumbwa wa Jimbo hilo, hivyo amewaomba mashirika ya kitawa kuboresha huduma za kiroho vijijini.

“Mashirika mengi ya kitawa wanaomba kusimamia parokia za mjini, niwaombe muende zaidi vijijini ili kuwaonjesha waamini upendo na huruma ya Mungu, kazi yenu ni kugusa mahangaiko ya watu” amesema

Matumaini ya askofu Msimbe ni kwamba Mashirika ya Kitawa watajipambanua kikamilifu kuongeza chachu ya imani kwa waamini jimboni Morogoro kama ambavyo huduma zao zimejikita kumhudumia mwanadamu kiroho na kimwili, ukilinganisha na huduma za elimu na afya wanazotoa katika jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *