Mhashamu askofu Lazarus Msimbe SDS wa Jimbo katoliki Morogoro amewakumbusha Utume wa Wanaume Katoliki Jimbo Katoliki Morogoro kuwa msitari wa mbele katika kulijenga kanisa la Mungu kuanzia ngazi ya familia, jumuiya, parokia na hatimaye Jimbo.
Askofu Msimbe amesema hayo katika sherehe ya kumuenzi somo wa Utume wa Wanaume Katoliki Jimbo Katoliki Morogoro mtakatifu Yosefu Mfanyakazi iliyofanyika katika Seminari ndogo ya mtakatifu petro Jimbo Katoliki Morogoro.
Askofu msimbe amefafanua kuwa ili kanisa la Mungu lisonge mbele lazima wanaume wawe wa kwanza kutimiza wajibu wao kuanzia ngazi ya malezi ya familia, kushiriki jumuiya ndogo ndogo za kikristo, na kuwasaidia wale wote wenye uhitaji wakiwemo mapadre wazee na wagonjwa ambao wanahitaji upendo wao.
Kwa upande wake mwenyekiti wa UWAKA Jimbo Katoliki Morogoro ndugu Anderson Mnyenyerwa ameahidi wao kama wanaume wakatoliki kuendelea kumsaidia askofu katika kutekeleza majukumu yake ikiwemo kusaidia kuwalea mapadre wazee na wagonjwa huku akieleza kuwa ili kuwafanya wanaume wote watimize majukumu yao wameandaa mpango kazi ambao utakuwa ndiyo muongozo wa utume wao.
