Askofu Msimbe: Kukua kwa Sayansi na Teknolojia kusirudishe nyuma dini na maadili.

Na Angela Kibwana, Morogoro.

Mhasham Askofu Lazarus Msimbe SDS, wa Jimbo Katoliki Morogoro amesema kukua kwa maendeleo ya sayansi na teknolojia kumesababisha baadhi ya watu kusonga mbele kidigitali na kurudi nyuma katika masuala ya imani hali inayofifisha misingi ya imani thabiti.

Askofu Msimbe amesema hayo wakati akitoa salamu na ujumbe wa Krismas kwa mwaka 2024 akisema kuwa kuzaliwa kwa Yesu Kristo iwe ni fursa ya ukombozi kwa watu wote ili waweze kutambua kwamba dini bila sayansi ni kiwete na sayansi bila dini ni kipofu.

Aidha katika mahojiano maalum askofu Msimbe amesema kuwa Sayansi na teknolojia vinategemeana na dini ambapo dini inahitaji sayansi na sayansi pia inaihitaji dini,hivyo kunahitajika weledi wa kutosha ili kupambanua mabo hayo.

Amesema kuwa watu wanazidi kusonga mbele zaidi katika maendeleo ya kiteknolojia, pamoja na maendeleo hayo ya kukua kwa sayansi amewahimiza waamini na watu wenye mapenzi mema kumuomba Mungu ili awajalie imani bila kuyumbishwa na maliwengu.

,,Sayansi imekwenda mbele zaidi kiasi kwamba dini imenyimwa nafasi na vitu vinavyotengezwa kitaalam na kisayansi vinawafanya watu washindwe kupata nafasi kumpa Mungu nafasi ya kusali, watu wako busy kutumia simu za mikononi kufuatilia vitu mbalimbali kwenye Luninga,, amesema Askofu Msimbe.

Ameongeza kuwa kwa nyakati za sasa watu wanapoteza muda mwingi zaidi kwenye mitandao ya kijamii na kukosa muda wa kusali na kufanya shughuli nyingine za kijamii zinazoweza kuwoangezea kipato, ambapo baadhi ya mambo wanayopata kwenye internet na mitandao ya kijamii zinawaharibu sana kimaadili

Amesema kuwa iko sababu ya kuendelea kuyachunguza mambo yasio na tija ikiwemo michezo ya kamali na tabia  kuangalia picha mbaya zinaathiri masuala ya imani, kwa hiyo watu wanapoharibika kimaadili wanazorota pia kimaadili.

Hata hivyo mamilioni ya watu wanaendelea kuishi kwa mahangaiko kwa sababu ya kukosa amani, hivyo askofu Msimbe amesema kuwa Kristu alimwaga damu kwa ajili ya amani ya dunia kwa kuwa amani ya kweli inapatikana kwa Kristo pekee, hivyo Krismasi iwasaidie waamini kutambua kuwa haki ndio iletayo amani ili wawe na moyo wa kusamehe na kupatanishwa na jirani zao kwa amani.

Amewahimiza waamini kumuomba Kristu mzaliwa akae kati yao ili kubadili hali zao za ubinadamu ifike kwenye utukufu wake ili sehemu zao za kazi ziwe Makanisa, kwenye madarasa ziwe ni sehemu za hija na hospitali zao ziwe mbingu kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu.

,, Kaa nasi Bwana utulize akili zetu mawazo na mioyo yetu inayohangaika, nyamazisha tamaa zetu mawazo na mioyo yetu inayohangaika na kurudisha roho zetu kwenye sura yako bila kukata tamaa,, Amesema askofu Msimbe.

Katika hatua nyingine askofu Msimbe amefafanua kuwa Krismas ni kipindi cha furaha kwa kuwa ili kuwa na furaha kunahitajika tunu ya Amani na upendo, na utulivu ili kila mmoja aweze kuwa na amani

Mwishoni mwa salamu zake amesisitiza watanzania kuendeleea kudumisha amani, mshikamano na maadili ili kila mmoja aweze kuifurahia Krismasi ikiwa ni pamoja na kuepuka vitendo vya uvunjifu wa amani bali kuwepo na utulivu ili kujipatanisha na Mungu na jirani zao pia na kutimiza mapenzi ya Mungu.

Mwisho

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *