Na Angela Kibwana, Morogoro.
Chuo cha Katekesi Mzumbe na Chuo cha Katekesi Bigwa Jimboni Morogoro wamefanya mahafali kuhitimisha kozi ya katekesi, ambapo wahitimu hao wamepata ujuzi wa kipekee katika lugha ya alama, ikiwa ni hatua muhimu katika kukidhi mahitaji ya Kanisa Katoliki kuwahudumia waamini wenye changamoto ya bubu na viziwi
Lugha ya alama itasaidia kuimarisha uwezo wa mawasiliano miongoni mwa kundi la waamini waliokuwa na changamoto ya kuongea na kusikia yaani bubu na viziwi ikiwa ni miongoni mwa kundi lililokuwa linakosa huduma za mafundisho ya Imani kutokana na ugumu wa kuwasiliana nao.
Jumla ya wahitimu 24 wa vyuo viwili vya Katekesi Jimboni Morogoro wamefanya mahafali ya kuhitimu masomo yao ya Katekesi ikiwa ni pamoja na kufuzu kozi maalum ya lugha ya alama ili kuendana na hitaji la Kanisa kwa sasa kutoa huduma kwa walemavu wa makundi mbalimbali.
Miongoni mwa wahitimu hao 24 kati yao wahitimu 16 ni kutoka chuo cha Katekesi cha Mtakatifu Karoli Lwanga Mzumbe na wahitimu 8 masista kutoka chuo cha Katekesi Bigwa ambapo Kanisa limepata rasilimali watu watakaofundisha Imani Katoliki.
Kupatikana kwa wataalam hao wa lugha ya alama ambao ni makatekista inawawezesha waamini wenye changamoto za mawasiliano kuelewa mafundisho ya Kanisa na kushiriki katika ibada na shughuli nyingine za Kanisa pamoja na kuondoa vizuizi vya mawasiliano na kuimarisha umoja.
Katika hafla hiyo ya kihistoria, Padre Dkt Listoni Lukoo, Mkuu wa Idara ya Katekesi Taifa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania,amesisitiza umuhimu wa lugha ya alama katika kutangaza Injili na kuwasaidia waamini walio na ulemavu bubu na viziwi
Amepongeza juhudi za Idara ya Katekesi Jimbo Katoliki Morogoro kuungana na Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) ili kuhakikisha kwamba haki na mahitaji ya watu wenye ulemavu wa kusikia yanatambuliwa na kutimizwa.

“Tuwape hongera sana Chavita Mkaoni Morogoro na Taifa kutambua umuhimu wa kozi hii katika Chuo cha Katekesi Mzumbe, nikushukuru sana padre Karoli na jimbo la Morogoro ninyi mmekuwa wa kwanza kutimiza azimio la mkutano kuzalisha wataalam wa lugha ya alama ndani ya Kanisa” alisema,
Padre Lukoo amesema katika mkutano wa mwaka wa idara ya Katekesi uliofanyika mwezi Aprili mwaka huu 2024 moja ya maazimio yake ilikuwa ni kuwaagiza wakuu wa vyuo vyote vya katekesi kuanzisha kozi ya lugha ya alama kuongeza wigo kumhudumia mwanadamu katika nyanja zote
Sambamba na hayo ameagiza uongozi wa chuo cha Katekesi Bigwa kinachosimamiwa na Masista wa Shirika la Moyo Safi wa Maria Morogoro, kufikia mwakani 2025 waanze kozi hiyo chuoni hapo ambayo italeta manufaa makubwa kwa Kanisa kwa kuwa masista hao wanapokea watoto wa makundi mbalimbali katika vituo vyao vya kulea watoto yatima ili iwe rahisi kuwasiliana nao.
Ametoa ushauri kwa uongozi wa Jimbo Katoliki Morogoro kuandaa mazingira rafiki kuwezesha wataalam hao wa lugha ya alama waendelee kubaki jimboni Morogoro ili waendelee kusaidia mafundisho ya Imani Katoliki badala ya kuajiriwa katika sekta nyingine.
Pamoja na hayo amewaomba makatekista hao kuwa waadilifu kushiriki ulinzi wa watoto kufuatia nyanyaso mbalimbali zinazowakumba watoto, akisema ziko kesi nyingi ambazo zimeripotiwa kuhusu vitendo vya ukatili wanaofanyia watoto
Sambamba na hayo padre Lukoo amepongeza wahitimu wa kozi hiyo ya lugha ya alama kuwa wa kwanza jimboni Morogoro na nchini, akisisitiza kuwa hiyo ni hatua ya kihistoria katika huduma ya katekesi na kuwasaidia waamini wenye ulemavu huo
Awali padre Lukoo amewapongeza wahitimu hao kwa kuhitimu kozi ya Katekesi iliyodumu kwa miaka miwili, ambapo Kanisa limeongeza waalimu wa dini katika nyanja mbalimbali za malezi huku akisema kazi ya ukatekista ni kazi ya majitoleo inayohitaji moyo wa sala na uaminifu zaidi katika utume.
Amewakumbusha maketekista hao kuwa na moyo wa toba kwa sababu bila kuwa na moyo wa toba kuna uwezekano mkubwa wa kuwa na moyo wa kisasi, ikiwa ni pamoja na kujenga kiburi, dharau na majivuno hivyo watambue kwamba bila kuwa na moyo wa toba watamkaribisha shetani.
Kwa mujibu wa padre Liston Lukoo Mkuu wa Idara ya Katekesi Taifa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania amesema kwa mwaka huu 2024 zaidi ya makatekesta 570 wamehitimu masomo ya Katekesi katika vyuo mbalimbali ili kukidhi hitaji la Kanisa kwa sasa.

Katika mahubiri yake kwenye adhimisho la Misa takatifu iliyofanyika katika parokia ya Mtakatifu Beda Bigwa Jimboni Morogoro, Makamu wa askofu Jimboni Morogoro padre Salvinus Kwembe amesema kuwa elimu ya lugha ya alama itawasaidia kuwasiliana na waamini wengi zaidi kwa kuwa Kanisa halikuwa na nyenzo za kuwasiliana na watu hao kukidhi mahitaji yao kimwili na Kiroho
Akitoa salamu na pongezi wa niaba ya askofu Lazarus Msimbe Sds wa Jimbo Katoliki Morogoro padre Kwembe amesifu juhudi na umahili wa padre Beatus Sewando mkurugenzi wa kituo cha Amani Morogoro kuwa na ujuzi wa kuwasiliana na walemavu wa kundi hilo kutekeleza matakwa na mahitaji yao ya kimwili na kiroho.
“Natambua ugumu wa kuwasiliana na walemavu wa aina hii kwa sababu sina utaalam wa lugha yao, ninapokutana nao au kuwasiliana nao napata shida, hatuelewani wala kusikilizana” amesema.
Hata hivyo amewakumbusha makatekista hao kuwa watu wa sala na tafakari na kupeleka injili nzuri kwa watu, na wala wasiishi kwa mazoea bali waige mfano wa Kristu kuwa wajumbe wa mwenyezi Mungu kuyaishi yote watakayofundisha pia wanaposali wasipayuke kama wanafiki
Kwa upande wake padre Karoli Mloka Ditenya mkurugenzi wa idara ya Katekesi Morogoro amesema wazo la kuanzisha kozi ya lugha maalum ya alama ilitoka kwa padre Liston Lukoo baadaye akamshirikisha padre Beatus Sewando wa Jimbo Katoliki Morogoro ambaye aliwezesha upatikanaji wa wataalam wa lugha hiyo waliokuwa wanafundisha maketekesta hao
Ameongeza kuwa Uwepo wa wahudumu wenye ujuzi wa lugha ya alama unasaidia kuongeza uelewa katika jamii kuhusu changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kukuza Imani yao hasa wanapoweza kuelewa mafundisho ya Kanisa na kushiriki katika ibada, wanapata fursa ya kukua kiroho
Naye padre Beatus Sewando Mkurugenzi wa kituo cha kulea watoto walemavu Amani Chamwino Morogoro kozi ya lugha ya alama itasaidia Kuimarishaujuzi wa lugha ya alama itakayochangia kuimarisha ushirikiano kati ya viongozi wa dini na waamini wenye ulemavu.
Amesema viongozi wa dini wanapokuwa na ujuzi huu, wanakuwa na uwezo wa kutoa mafundisho ya Kanisa na huduma kwa usahihi, na hivyo kujenga mazingira bora ya kiroho.
Kwa ujumla, uwepo wa lugha ya alama ni muhimu katika kuimarisha ushirikiano, uelewa, na huduma ndani ya Kanisa na jamii, na unachangia katika kukuza imani na uhusiano wa karibu kati ya waamini wote, bila kujali changamoto zao.
Padre Sewando ametoa mwaliko kwa makundi mbalimbali kutoka majimbo yote Katoliki 34 nchini Tanzania kuzalisha wataalam wa lugha ya alama ili kuendana na misingi ya Kanisa katoliki katika kumhudumia mwanadamu kimwili na kiroho kwa kuwa katika maadhimisho mbalimbali ndani ya Kanisa kundi la walemavu wa aina hiyo wanakosa fursa ya kuelewa neno la Mungu
Malengo Makuu ya kuanzisha kozi hio ni Kutetea Haki za walemavu kwakuweka mbele masuala ya haki za viziwi, kuhakikisha wanapata huduma bora, elimu, na fursa za ajira,kukuza ushirikiano kati ya wanachama, mashirika ya serikali na yasio ya kiserikali ili kutatua changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu wa kusikia.
mwisho