Kampeni ya msaada wa kisheria ya mama Samia yaleta kicheko kwa wanyonge.

Na Angela Kibwana, Morogoro.

Waziri wa Katiba na sheria Dk Damas Ndumbaro amezindua rasmi kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Mkoani Morogoro, ikiwa ni mkoa wa 11 tangu kuanza mpango huo wa msaada wa kisheria unaolenga kuwasaidia watanzania wasio na uwezo.

Dkt Ndumbaro amesema hayo katika uzinduzi wa kampeni hiyo Desemba 13 mwaka huu mkoani Morogoro ambapo utekelezaji wa kampeni ya msaada wa kisheria ya mama Samia unatokana na irani ya Chama cha Mapinduzi CCM ya mwaka 2020 kitabu chenye kurasa 303.

Amesema katika irani hiyo chama cha Mapinduzi kiliwaahidi Watanzania kuwapa msaada na huduma za kisheria kwa ukaribu zaidi na gharama nafuu, hivyo kuzinduliwa kwa kampeni hiyo ni utekelezaji ambao chama cha mapinduzi kupitia serikali yake ilipanga kuyatekeleza.

Amesema kuwa mkakati huo unatokana na utekelezaji wa sheria ya utoaji wa msaada wa  sheria ya mwaka 2017, ambapo wabunge wa bunge wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania walitunga sheria ya utoaji wa msaada wa kisheria ambayo itawasaidia wananchi wasiojiweza kupata huduma za msaada wa kisheria.

,, Dkt Samia Suluhu hasani ni Rais mwenye sifa kemkemu ni mama muungwana sana anayewafikiria watanzania walio wanyonge, ndio maana amekuja na kampeni ya msaada wa kisheria kwa watanzania wote katika pande mbili za jamhuri ya muungano wa Tanzania,tangu achukue majukumu ya kuongoza nchi marchi 19 mwaka 2021 nchi inasonga mbele kwa kila eneo,, amesema Dkt Ndumbaro.

Aidha Morogoro ni mkoa wa pili kwa ukubwa hapa nchini, ukiwa na ukubwa wa Kilomita za mraba 72,939 na wakazi 3,197,104 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022 ukiwa ni mkoa wa uhifadhi, ufugaji na mkoa wenye sifa za kuwa ni ghala la chakula, hivyo migogoro mingi iliokuwa inajitokeza kati ya wakulima na wafugaji,itapatiwa ufumbuzi wa wataalam wa sheria ambao watadumu kwa siku 9 kuanzia Disemba 13-22 mwaka huu 2024. 

Amesema kuwa kumuona mwanasheria ni gharama kubwa ambazo zimekuwa zikisababisha wananchi wasio na uwezo kushindwa kutatuliwa changamoto zao, hivyo Rais Dkt Samia ametuma  wanasheria mkoani Morogoro kusikiliza wananchi na kutoa elimu bure ili kutoa haki kwa watanzania wote.

Amebainisha kuwa mkoa wa Morogoro unakabiliwa na matatizo ya ndoa, mirathi, migogoro ya ardhi kwa wakulima na wafugaji, huduma na msaada wa changamoto hizo zitatolewa bure ili wananchi waweze kunufaika na kampeni hiyo.

Baada ya kuzinduliwa kwa kampeni hiyo mkoani Morogoro, Dkt Ndumbaro anatarajia kuzifikia Halmashauri zote 9 na wilaya 7 za mkoa huo ili kuhakikisha wananchi wanyonge wasio na elimu ya kisheria wala uwezo wa kulipia gharama za mawakili watafikiwa na huduma hizo za msaada wa kisheria huko huko waliko bila gharama yoyote.

Amesema kuwa katika kampeni hiyo ya msaada wa kisheria ya mama Samia haiangalii tu sheria bali wanajikita katika utoaji haki kwa wananchi wote kwa kuzingatia usawa ili wakulima, wafugaji na wafanya biashara waweze kuona namna serikali inavyowajali kwa maendeleo ya taifa.

Amesema kuwa jamii yenye haki inakuwa na usawa, hivyo kukosekana kwa usawa ni chanzo cha kutoheshimiana, kukosekana kwa uvunjifu wa amani, kwa sababu uwepo wa haki na usawa kunakuwa na Amani, hivyo kampeni hiyo inalenga pia kupigania haki ili kulinda na kuendeleza amani iliopo tangu kupatikana kwa uhuru

,,Tukiwa na haki, usawa na amani inazaa maendeleo sehemu ambayo haina haki, usawa, na amani haiwezi kuwa na maendeleo, kwa sasa nchi inasonga mbele kimaendeleo kwa sababu kuna haki usawa na amani,ndio maana Rais Samia ameleta msaada wa kisheria ili kuhakikisha mambo yanaendelea,, ameeleza Dkt Ndumbaro.

,,Tusifikirie Migogoro tufikirie kulima, tusifikirie migogoro tufikirie kufuga, tufikirie fursa za uzalishaji viwandani, utaliii, biashara na kusafiri kwa raha mstarehe kupitia treni ya SGR ambayo ni tunu waliojaaliwa watanzania,, ameeleza

Amesema kuwa kampeni hiyo sio tu ya mkoa wa Morogoro bali ni kampeni ya kitaifa inayokwenda katika mikoa yote nchini ili kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi

Mpaka sasa kampeni hiyo imepita katika mikoa ya Dodoma, Manyara, Singida,Songwe, Shinyanga, Simiyu, Mara, Ruvuma, Njombe na Iringa ambapo Morogoro ikiwa ni Mkoa wa 11 tangu kuzinduliwa rasmi kwa kampeni hiyo.

Kampeni hiyo ina malengo makuu manne ambayo ni kuongeza uelewa wa masuala ya kisheria na haki za binadamu kwa jamii hususani haki za wanawake na watoto, kuimarisha huduma za ushauri wa kisheria kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia, kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu elimu ya sheria kwa umma masuala ya haki na wajibu pamoja na misingi ya utawala bora.

Malengo mengine ni kutoa elimu ya usimamizi wa mirathi urithi, sheria ya ardhi na haki ya kumiliki mali, utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala hususani kwa viongozi wa serikali za mitaa, watendaji wa kata, vijiji na wajumbe wa mabaraza ya ardhi kwa kushirikiana na wazee maarufu, machifu, na viongozi mbalimbali wa dini na serikali

Malengo hayo lazima yatekelezwe na kila mmoja kuanzia ngazi ya familia, mtaa, kata na wilaya ikiwa ni pamoja na viongozi wa dini na taasisi mbalimbali mkoani Morogoro

Kampeni hii itakuwa ni fursa katika mkoa wa Morogoro  ambao unapakana na mikoa 8 wenye makabila mbalimbali yenye tamaduni na shuguhuli za kiuchumi zinazofanywa na wananchi ambazo zimekuwa zikisababisha uwepo wa migogoro mingi ya wakulima na wafugaji

Dkt Ndambaro amesema kuwa kupitia kampeni hayo inatarajiwa kukomesha migogoro ya uharibifu wa mazingira mkoani humo kwa sababu Morogoro ndio makao makuu ya uhifadhi wa mazingira ambapo 81% ya maji yanayokwenda kwenye Bwawa la kufua umeme la mwalimu Nyerere hutoka katika mkoa wa Morogoro.

Kampeni ina malengo ya kupima matokeo baada ya kampeni hiyo mojawapo ikiwa ni kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu masuala ya haki mifumo ya kisheria iliyopo, haki za binadamu na haki za makundi maalum, Kuboresha mifumo ya utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala na masuala ya upatikanaji haki kwa ujumla.

Kampeni hiyo inalenga pia kulinda na kukuza haki kupitia msaada wa kisheria, kuboresha upatikanaji wa haki kwa wasio na uwezo wa kumudu gharama za huduma za kisheria hasa wanawake, watoto, wazee , walemavu na makundi mengine yalio katika mazingira magumu na hatarishi, kuimarisha amani na utulivu na ustawi wa jamii.

,,Malengo hayo yakitimia Tanzania itakuwa ni nchi salama yenye amani na utulivu na maendeleo zaidi, amani na utulivu haishuki kama Mana kutoka mbinguni, na sisi ni lazima tufanye juhudi kulinda amani na utulivu,, amesema Dkt Ndumbaro.

Alisema kuwa ibara ya 28 ibara ndogo ya katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania inasisitiza kuwa ni jukumu la kila mtu kuchangia katika Amani, utulivu na maendeleo ya nchi.

Wakati huo huo Dkt Ndumbaro amesema kuwa kufuatia masuala ya ukatili wa kijinsia ambalo limekuwa donda ndugu linaloendelea kuathiri wahanga wa vitendo hivyo, kampeni hiyo ya msaada wa kisheria wa mama Samia inatarajia kukomesha na kutoa elimu au mbinu za kukabiliana ubakaji, ulawiti mimba za utotoni na manyanyaso dhidi ya wanawake.

Ametoa rai kwa viongozi wa dini, mila ikiwa ni pamoja na wazazi na walezi kwa sababu serikali ikinyooshewa vidole kwamba inafanya nini maadili yanazidi kumomonyoka, huku ukatili wa kijinsia ukiendelea kushamiri ndani ya jamii, hivyo suala la elimu ya maadili sio la serikali bali linapaswa kuwa ajenda inayoanzia nyumbani, taasisi za dini na sehemu za makazi mbalimbali ambalo linapaswa kukemewa kikamilifu ili kuilinda jamii ya kitanzania.

,,Tukemee unyanyasaji na ukatili wa kijinsia, tufuatilie mienendo  ya watoto wetu lakini tufuatilie pie mienendo ya mafilauni pia ili tujue nani ni filauni ili tumpe anachostahili tuilinde jamii ya kitanzania ili iwe salama,,

Amesema wizara inahitaji kufanya maboresho mbalimbali katika mifumo ya sheria, hivyo ametoa agizo kwa katibu mkuu, watendaji na taasisi zote  za wizara kuboresha mabaraza ya kata, ambapo kwa mujibu wa sheria ya mabaraza ya kata ya mwaka 1985 sura ya 206 kuna baraza la  katika kila kata ndani ya Tanzania bara

Amesema mabaraza hayo ni chombo muhimu sana cha usuluhishi wa migogoro na matatizo mbalimbali katika jamii, endapo kama yangefanya kazi vizuri migogoro na matatizo mengi yasingetokea,jamii imekuwa ikipata matatizo kwa sababu mabaraza hayo hayafanyi vizuri

Dkt Ndumbaro ametoa agizo mabaraza hayo yafanyiwe tafiti na kuweka mapendekezo serikalini ili kufanya mabadiliko makubwa kwenye mabaraza hayo ya kata yaweze kuendana na wakati kutoa huduma kwa wananchi wote wa Tanzania.

Mwishoni ametoa shukrani kwa katibu mkuu wa Wizara ya katiba na sheria Eliakim Chacha pamoja na timu yote na taasisi zote zilizopo chini ya wizara kwa kuandaa na kuratibu vizuri kampeni hiyo ambayo hadi sasa imefika katika mikoa 11 huku akiwashukuru wadau wote walioshiriki utoaji huduma ya msaada wa kisheria kuendeleza ushirikiano na serikali ili msaada huo wa kisheria uwe endelevu na kuongeza mafanikio katika kona zote za Tanzania.

Mwisho

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *