Na Angela Kibwana, Morogoro.
Askofu wa Jimbo Katoliki Morogoro Mhashamu Lazarus Msimbe SDS amezindua rasmi jubilei kuu ya uinjilishaji miaka 2025 ya Ukristo ngazi ya Jimbo, baada kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis kufanya uzinduzi huo Desemba 24 wakati wa mkesha wa Krismasi katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Roma.
Baada ya Papa Francis kufanya uzinduzi huo alitoa mwaliko kwa Kanisa la ulimwengu mzima majimbo yote kufanya uzinduzi decemba 29 mwaka huu ambapo kwa jimbo la Morogoro Misa za dominika zilifanyika desemba 28 kwenye parokia zote ili waamini waungane na kanisa zima kushiriki uzinduzi wa mwaka Mtakatifu wa jubilei.
Askofu Msimbe amefanya uzinduzi huo katika Kanisa la Bikira Maria mama wa Kanisa Kigurunyembe Jimboni humo badala ya kufanyika katika kanisa kuu la Mtakatifu Patris kutokana na shughuli za ukarabati zinazoendelea Kanisani hapo.

Askofu Lazarus Msimbe SDS akiongoza maandamano ya uzinduzi Jubilei ya miaka 2025 Kijimbo
Katika mahubiri yake askofu Msimbe amesema kuwa maadhimisho ya mwaka wa jubilei iwe ni fursa ya kuvua magamba ya dhambi na kujibidiisha zaidi katika hali ya kufanya toba ili kuwawezesha waamini kupata rehema kamili.
Awali kabla ya kuanza adhimisho hilo ilitangulia ibada fupi iliyofanyika katika kanisa la zamani la Kigurunyembe TTC ikifuatiwa na maandamano yaliotanguliwa na msalaba kwa kuwahusisha makrelo, waamini waliofurika kushuhudia uzinduzi huo na kujichotea baraka.
Baada ya kufika kwenye kanisa jipya la Bikira Maria mama wa Kanisa, askofu Msimbe alifungua mlango wa Kanisa na kubusu msalaba kama ishara ya kuingia katika huruma ya Mungu yaani kuachana na dhambi nje na kuingia ndani kwenye neema .

Makrelo,watawa na waamini waliojitokeza katika Kanisa jipya la Bikira Maria Mama wa Kanisa Kigurunyembe wakishiriki misa takatifu ya uzinduzi Jubilei 2025
“Kuhusu rehema za jubilei ya miaka 2025 ni njia ya hija ambayo inawataka waamini kufanya hija zaidi ya kiroho, kama mlikuwa hamjui Kanisa la Mtakatifu Yohane Laterano ndio Kanisa mama ya makanisa yote ulimwenguni mlango wake umefunguliwa decemba 29 2024 wakati makanisa yote duniani yanafanya uzinduzi kwa kufungua milango yake” amesema askofu Msimbe.
Amewahimiza waamini kupyaisha maisha yao kwa kufanya hija katika maisha yao ya kiroho kwa njia ya sala, kuwaombea maskini na watu wenye shida mbalimbali ili kujitakasa kiroho kwa kutembelea makanisa ya hija yaliopo jimboni humo.
Mbali na kufanya hija askofu Msimbe amehimiza waamini kufanya matendo ya huruma kwa wahitaji wakati wa maadhimisho haya ya jubilei ya uinjilishaji miaka 2025 ya ukristo, kufanya mafungo, sala, maungano kujipatanisha na Mungu kwa kupokea sakramenti ya upatanisho wanapokwenda kukutana na Mungu.
Sambamba na hayo askofu Msimbe amewakumbusha waamini kujinyima matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii kuwa makini na mitandao hiyo kwa sababu baadhi ya waamini wamekuwa dhaifu kudhorotesha shughuli zao za uzalishaji kwa sababu ya kupoteza muda mwingi kwenye mitandao hiyo.

“Tunatakiwa kujinyima kabisa kwenye mitandao ya kijamii tuwe makini nayo, kuna wengine wamezama zaidi kwenye matumizi ya mitandao ya kijamii, kuna wengine wamepotea na kuzama kwenye Whatsapp, Tiktok, hata muda muda wa kusali hana, mitandao ya kijamii inashawishi lakini tujipe muda wa kusali
Katika hatua nyingine amewaomba waamini kutumia mitandao ya kijamii kwa umakini kwa mambo ya kiroho hasa uinjilishaji endelevu, na kuwaomba waamini kujipa muda wa kusali, na kufanya mafungo kwa mapadri na waamini
Jambo lingine la kufanya wakati wa maadhimisho hayo ni kuwalinda watoto, kuwaheshimu wazee, kuwasaidia maskini na wahitaji, kuwapokea wahamiaji na kulinda uhai wa binadamu kwa kuepuka masuala ya utoaji mimba.
Amehimiza mapadri kubuni mbinu za kuongeza wigo wa mafundisho, semina za kiroho katika vigango na parokia zao, kitubio kwa waamini ili kuwasaidia waweze kumjua Mungu na kumpenda zaidi

Kilele cha maadhimisho hayo ya mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya miaka 2025 ya Ukristo kwa majimbo yote itakuwa ni Desemba 28 mwaka 2025 ambapo Papa Francis atafunga rasmi maadhimisho hayo januari 6 mwaka 2026 katika Kanisa la Mtakatifu Petro Mjini Roma.
Mwishoni amezindua sala ya jubilei ya miaka 2025 ya ukristo ambayo itakuwa inasaliwa mwishoni mwa misa kabla ya Baraka, ikiwa ni pamoja na kutoa rehema kamili kwa waamini walioshiriki adhimisho hilo
Kauli mbiu inayoongoza maadhimisho hayo ni “Mahujaji Katika matumaini”
Mwisho