Mahakama kuu kanda ya Morogoro yajipanga kuleta mabadiliko chanya kufanikisha malengo ya kitaifa 2050.

Na Angela Kibwana, Morogoro

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu kanda ya Morogoro Stephen Murimi Magoiga amesema elimu ya wiki ya sheria kwa kanda ya Morogoro imewafikia wananchi 23,310 kwa kupewa elimu ya sheria na haki mbalimbali kati yao wanawake ni 6,970 wanaume 6,234 na watoto wanafunzi wakiwa ni 10,106 ambapo idadi hiyo haihusishi elimu iliyotlewa kwa njia ya vyombo vya habari.

Amesema hayo katika maadhimisho ya siku ya sheria nchini iliyokwenda sambamba na uzinduzi wa mwaka mpya wa mahakama  iliyofanyika katika kituo jumuishi cha Utoaji haki IJC Mkoani Morogoro na kuwashirikisha wadau mbalimbali wa haki mada ikiwemo  viongozi wa dini na watu mbalimbali.

Aidha Mh. Murimi alisema kuwa Mahakama ya Tanzania ni muhimili pekee wa dola uliopewa mamlaka ya utoaji haki, kwa hiyo kwa kuzingatia wajibu huo Mahakama ya Tanzania inaongozwa na dira isemayo utoaji haki kwa wakati na kwa watu wote.

Kwa hiyo katika kutekeleza  hilo kila mwaka Mahakama huadhimisha siku ya sheria kabla ya kuanza majukumu yake ili kupata nafasi ya kueleza watanzania ambao ndio watumiaji wa huduma za mahakama juu ya shughuli zilizofanyika mwaka ulioisha na kutambua mipango iliyopo na kufungua rasmi mwaka mpya wa mahakama.

Mahakama ya Tanzania imeendeleza utamaduni wake kwa kipindi cha miaka 11 mpaka sasa tangu kuanzishwa kwa wiki ya sheria 2014 kuwa na kauli mbiu inayosimamia shughuli na utaratibu mzima wa wiki ya sheria, ambapo katika siku ya sheria nchini kila mwaka kunakuwa na kesi ya mfano kusikilizwa siku ya kuanza shughuli hizo za mahakama .

Mheshimiwa Murimi alisema kupitia kauli mbiu ya mwaka huu 2025, wadau wa haki madai kuhakikisha wanashirikiana kutoa maoni ya mambo muhimu ya kisheria na nyanja nyingine yatakayosaidia kufikisha azma ya serikali katika kufikia dira ya taifa ya  maendeleo 2050.

“Sisi kama wadau wa haki madai tunajitathmini na kuweka mikakati ya pamoja kama wadau wa mahakama na namna gani tunaweza kushirikiana bila kuingiliano katika kuhakikisha kwamba dira ya taifa ya maendeleo inatekelezwa na malengo yake kufikiwa kikamilifu”, alisema Magoiga.

Aliongeza kuwa siri ya mafanikio ya taifa imefichwa kwenye haki, na kwa kuwa upatikanaji ni mnyororo unahitaji kila taasisi kutekeleza wajibu wake ipasavyo hivyo Mahakama ya Tanzania inawataka wadau wa haki madai kufahamu juu ya Tanzania inayohitajika 2050 kujipanga kikamilifu namna wanavyoweza kutekeleza majukumu yao na kuiwezesha mahakama kutekeleza wajibu wake kwa usahihi pale inapofikiwa na wananchi wanaohitaji msaada wa haki

“Kinyume cha haki ni dhuluma na nia adui wa maendeleo ya mtu mmojammoja na taifa kwa ujumla,leo tumejumuika hapa ili kudumisha dhamira ya kuimarisha utawala wa sheria haki, Maendeleo ya jamii na kiuchumi katika taifa kusukuma gurudumu la maendeleo

Naye mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima ameipongeza mahakama kuu Tanzania kuadhimisha siku muhimu ya sheria katika mustakabali wa masuala ya utawala wa sheria, ustawi wa kiuchumi, kijamii na kisiasa katika taifa.

Alibainisha kuwa muhimili wa mahakama una nafasi katika utekelezaji wa majukumu yao kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya haki ili kuongeza tija na usawa bila upendeleo wowotehivyo hakuna maendeleo yatakayoweza kupatikana bila usimamizi mzuri wa haki na sheria dhidi ya wananchi

“Serikali ya mkoa wa Morogoro inatambua mchango wa wadau wote wa taasisi za mahakama kwamba tunathamini ushirikiano uliopo kwa ajili ya manufaa ya watanzania wenzetu”

Alisema kuwa Mkoa wa Morogoro kwa muda mrefu unakabiliwa na changamoto ya migogoro ya wakulima na wafugaji, ardhi na mashamba, ukatili wa kijinsia, migogoro ya familia na mirathi, ukatili wa watoto, ngono, changamoto za rushwa na ubadhilifu wa miradi ya umma, changamoto za uzembe na uwajibikaji kwenye utoaji wa huduma za umma ambapo zinahitaji msaada wa kimahakama.

Kuna migogoro ya wivu wa mapenzi , vitendo vya ulawiti na ubakaji ndani ya jamii, haya yote yanapaswa  kutafsiriwa kisheria na matendo , hivyo siku hii ya sheria isaidie kutafakari mafanikio ya mahakama kuu Tanzania

Sambamba na hayo Mkuu huyo wa Mkoa Adam Malima aliahidi kuonesha ushirikiano kupinga vitendo vya unyanyasaji na ukatili dhidi ya wasichana wanaonyimwa haki zao msingi za elimu, akisema popote mtoto wa kike atakaponyimwa haki yake katika mkoa wa Morogoro halitakubalika nakuomba ushirikiano wa mahakama utakapobaini kesi ya ukatili wa kijinsia wahusika wachukuliwe hatua ili kupunguza matukio ya unyanyasaji wa watoto na watu wenye ulemavu kuboresha upatikanaji wa haki.

Maadhimisho hayo ya siku ya sheria yalianza rasmi tarehe 01 Marchi mwaka 1996, kipindi hicho sherehe hizo ziliadhimishwa kwa kuanza kusikiliza mashauri yaliotokana na uchaguzi wa kwanza uliohusisha vyama vingi mwaka 1995, hivyo mkutano wa waheshimiwa majaji na wasajili mwaka 1996 kwamba kuwe na mwendelezo wa siku ya sheria itakayoadhimishwa mwanzoni mwa mwezi februari kila mwaka

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *