Rais Dkt Samia atoa shilingi milioni 100 kukarabati Kanisa Kuu la Mtakatifu  Patris Morogoro.

Na Angela Kibwana, Morogoro.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan amechangia shilingi Milioni 100 kuunga mkono juhudi shughuli za ukarabati wa Kanisa kuu la Mtakatifu Patris Jimboni Morogoro ambalo linakabiliwa na uchakavu wa miundombinu tangu kujengwa mwaka 1961.

Mhasham Lazarus Msimbe sds askofu wa Jimbo Katoliki Morogoro akitoa shukrani mbele ya waamini wa Kanisa kuu la Mtakatifu Patris jimboni humo iliyofanyika katika kituo cha mafunzo Social Education Centre amesema Rais Samia ametoa fedha hizo kwa ukarimu ili kuungana na waamini wa Kanisa kuu na watu wenye mapenzi mema wanaoendelea kuchangia ukarabati wa Kanisa hilo.

Amesema kuwa kwa kutambua umuhimu wa jambo hilo baada ya kuona jitihada za kukarabati wa Kanisa hilo, Rais Samia ametoa fedha hizo shilingi milioni 100 kufanikisha ukarabati wa Kanisa hilo jambo ambalo limegusa hisia za waamini wengi Kanisani hapo.

Pichani ni Askofu Lazarus Msimbe alipofanya ziara kukagua ukarabati wa kanisa hilo.

Askofu Msimbe amesema kuwa kabla na mara baada ya kuanza kwa ukarabati huo amejaribu kuomba ufadhili hata nje ya nchi bila mafanikio yoyote, hivyo amesema kuwa Rais Samia ameonesha ukarimu mkubwa kushiriki ujenzi wa nyumba ya Mungu.

“Kumbe ukianza kufanya jitihada mwenyewe watu wanakuona, hatujawahi kupata mchango mkubwa kama huu katika harakati za kuchangia ukarabati wa Kanisa letu,  kama nilivyosema nilishawahi kuomba kwa wafadhili nje ya nchi lakini sikufaulu, Namshukuru sana Rais Samia kwa mchango huu mkubwa kwetu”

Aidha askofu Msimbe amesema kuwa ukarabati wa Kanisa hilo unahitaji kiasi cha shilingi Mil. 650 za Kitanzania,ambapo hadi kufikia mwezi Oktoba michango iliotolewa imefikia asilimia 45 ya pesa zinazohitajika ifikapo oktoba.

Askofu Msimbe akielezea namna ya muonekano wa kanisa hilo pindi ukarabati utakapo kamilika .

Amewaomba wadau mbalimbali ikiwemo viongozi wa serikali na waamini kwa ujumla kuendelea kutoa michango yao kwa ajili ya ukarabati wa Kanisa hilo ili kazi hiyo iweze kukamilika mapema kwa muda uliopangwa.

Kwa sasa wakandarasi wako kazini ikiwa tayari kuta za mbele zimebomolewa kuanza rasmi kuunda mwonekano mpya wa Kanisa hilo ili liweze kuwa na mwonekano wa kisasa ukilinganisha na lilivyokuwa awali katika muundo wa box.

“Nadhani sote ni mashahidi tunaona kazi inayoendelea hapa Kanisani awamu ya kwanza ya ukarabati ili kazi hiyo iweze kukamilika tuweze kukaa kwenye  nyumba za Mungu inayompendeza Mungu na sisi wenyewe tunaosali,sura ya mbele inaokenana vizuri  na kumekuwa na mabadiliko ya kasi sana, namshukur tena Rais Samia Mungu ambariki Rais, abariki Jimbo letu na Taifa la Tanzania” amesema.

Kwa upande wake Michael Simeo Maghembe mwenyekiti Halmashauri walei Parokia akisoma taarifa fupi ya ukarabati wa Kanisa hilo amesema kampeni ya ukarabati huo ilizinduliwa rasmi na askofu Lazarus Msimbe Agosti 22, mwaka 2023

Tangu wakati huo waamini walianza rasmi kuchangia kwa njia mbalimbali kukusanya fedha za kukarabati Kanisa ikiwemo kampeni ya harambee ya picha ambayo imewezesha makusanyo ya kiwango kikubwa kupata fedha.

Tangu Agosti 22 mwaka jana 2023, hadi kufikia mwezi Oktoba mwaka huu 2024waamini hao wamechanga fedha jumla ya shilingi Mil.189,832,150 zilizofanikisha hatua za awali kuanza ukarabati wa jengo hilo ambapo hadi sasa shilingi milioni 81,863,603 kwa ajili ya kununua vifaa vya ujenzi na gharama za awali kulipa mafundi

Amewashukuru waamini wa parokia hiyo na watu wenye mapenzi mema kwa mshikamano wa dhati kushikamana katika ukarabati wa Kanisa hilo la kiaskofu Jimboni Morogoro

Kwa sasa waamini wa Kanisa hilo wanasalia katika ukumbi wa kituo cha mafunzo Social Education Centre kilichopo jirani na Kanisa hilo, ambapo kulingana na ufinyu wa eneo hilo wamelazimika kuongeza idadi ya Misa,na huduma nyingine za ibada mbalimbali kwa siku za kawaida zinafanyika katika ukumbi wa Kanisa hilo.

Muonekano wa ndani wa kanisa kuu la Mtakatifu Patris

Ukarabati wa Kanisa hilo unakwenda sambamba na ujenzi wa grotto ya Mama Bikira Maria,pamoja na mnara wa kengele.

Ujenzi wa kanisa hilo unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Oktoba mwaka 2025.

Wadau na watu mbalimbali wenye mapenzi mema wanahitajika ili kukamilisha kwa wakati ukarabati huo, Michango hiyo inakusanywa kwa akaunti ya Mkombozi Banki – ACC NO: 00721818144901 Jina –Mfuko wa Halmashauri walei parokia ya Mtakatifu Patrick Morogoro.

Au michango hiyo inapokelewa kwamfumo wa LIPA KWA SIMU NO: 5176653- JINA MTAKATIFU PATRIS JIMBO KATOLIKI MOROGORO

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *