Wajibu wa Kanisa kwa watu wenye ulemavu katika  huduma za Kiroho

Kanisa ni jumuiya ya waamini wanaomwamini Yesu Kristo, Kanisa ni mwili wa kristo ambao kristo mwenyewe huulisha na kuutunza, hivyo waamini wa kanisa nao ni mwili wa Kristo kwa kuwa kwa neno lake Kristo wanalishwa na kutunzwa (Waefeso 5: 29 na Wakolosai 1: 24). Kristo ni kichwa cha mwili, yaani Kanisa (Wakolosai 2:10).

Kanisa Katoliki ni kichwa na mwili wa Kristo, ambalo asili yake ni Kristo mwenyewe, aliyemteua mtume Petro kuwa Kiongozi wa kwanza wa kanisa katoliki (Mathayo 16:18)

Katika majukumu yake kanisa katoliki linao wajibu muhimu kwa waamini wake na jamii kwa ujumla.

Majukumu haya yanaweza kugawanywa katika vipengele vya kiroho na kimwili yaani kijamii, kielimu, na kihisia).

Katika mtazamo wa mahitaji ya kimwili Yesu Kristo ambaye ni kichwa na mwili wa kanisa alipata kuwafanya vipofu kuona, wenye ukoma kutakasika,Viziwi kusikia, wafu kufufuliwa, na masikini kuhubiriwa (Luka 7:22).

Jambo hili linaweza kuwa na maana zaidi kiroho, lakini kwa muktadha  wa kudhihirisha Kristo yuko ndani yetu na anatenda kazi alishughulikia mahitaji ya mwili  sio zaidi kwa ajili wenye miili  bali kwa matendo yaliyo mema, ili watu wa Mungu wapate kuokolewa na neema zake zidhihirike ( Wafilipi 1:21)

Kwa jumla, pamoja na jukumu la kiroho ambalo ni kueneza Injili, kujenga jumuiya  na kufundisha mafundisho ya Kikristo ili kuimarisha imani ya waamini  kanisa Katoliki  lina majukumu mengine  yafuatayo: Kutoa Huduma za Kijamii, Kukuza Amani na Haki, Kutoa Elimu, Kuwa Mwangaza wa Maadili, Wajibu wa Kihisia na Kisaikolojia majukumu ambayo kanisa limeyatekeleza na linaendelea kuyatekeleza kwa ufanisi mkubwa sana.

Msingi wa utekelezaji wa jukumu kuu la uinjilishaji ni mawasiliano kwa lugha ya sauti na matendo ili kuwafikia watu wote Ulimwenguni kama alivyo agiza Kristo Yesu mwenyewe kwa mitume wake “ Enendeni Ulimwenguni mwote mkahubiri Injili kwa kila kiumbe” (Marko 16:15).

Kwa kutambua kuwa viumbe wote ni wa Kristo, na uwepo wa makundi yenye mahitaji maalum katika jamii kama vile watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na ulemavu wa kusikia na kuongea,na kwa kutekeleza agizo la Bwana Yesu Kristo (Marko 16:15) Kanisa la duniani lina wajibu wa kuyafikia makundi hayo kulingana na mahitaji yao.

Katika mazingira mengi, upatikanaji wa Neno la Mungu na mafundisho ya Kanisa kwa kundi hili umekuwa changamoto kubwa kutokana na ukosefu wa mawasiliano ya moja kwa moja kati yao na viongozi wa dini pamoja na waamini wenzao.

Hali hii inazua maswali mengi na kuongeza msukumo wa umuhimu wa viongozi wa Kanisa kujifunza na kutumia lugha ya alama ili kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wa kusikia wanapata huduma za  kiroho kama waamini wengine.

Katika mafundisho ya Kanisa, kila mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na anayo haki ya kushiriki kikamilifu katika maisha ya kiroho, hii ni pamoja na kupokea sakramenti, kushiriki ibada, na kufundishwa Neno la Mungu.

Watu wenye ulemavu wa kusikia wanapokosa huduma hizo kutokana na changamoto za mawasiliano,wanakosa nafasi ya kujijenga kiroho na kufurahia mshikamano wa Kanisa,hii inaweza kupelekea kujiona wamesahaulika au kutengwa, jambo ambalo linapingana na ujumbe wa upendo na ujumuishi wa Kikristo pamoja na agizo la kristo mwenyewe (Marko 16:15)

Pamoja na jitihada za Kanisa kufikia makundi yote, bado kuna pengo kubwa katika huduma kwa viziwi na bubu ambapo katika ibada nyingi, hakuna wakalimani wa lugha ya alama, na viongozi wa dini wengi hawana ujuzi wa kuwasiliana na kundi hili.

Changamoto  hii inasababisha  uelewa mdogo kwa mafundisho ya imani, ukosefu wa mshikamano wa kiroho, na hatimaye kuwafanya watu wenye ulemavu wa kuongea na kusikia  yaani viziwi na bubu kuhisi wamesahauliwa na Kanisa.

Moja ya changamoto kubwa zinazokwamisha huduma za kiroho kwa watu wenye ulemavu wa kusikia ni ukosefu wa mafunzo ya lugha ya alama kwa viongozi wa dini kwa sababu katika seminari nyingi na vyuo vya malezi ya kichungaji, lugha ya alama haifundishwi kama sehemu ya mitaala.

Kwa hiyo changamoto hiyo inawafanya mapadre, masista, na viongozi wa jumuiya za Kikristo kushindwa kuwasiliana ipasavyo na kundi hili, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vifaa na rasilimali zinazoweza kusaidia mawasiliano,kama vile vitabu vya ibada vilivyotafsiriwa kwa lugha ya alama au teknolojia za kisasa zinazoweza kusaidia kufikisha ujumbe wa Injili kwa njia zinazoweza kueleweka na watu wenye ulemavu wa kusikia.

Watu wenye ulemavu wa kusikia mara nyingi hukumbana na unyanyapaa, na baadhi ya watu wanaweza kuona kwamba hawawezi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiroho hivyo waamini wanapaswa kubadili mitazamo yao kuanza kuwashirikisha watu wenye ulemavu katika masuala ya Kiroho.

Kwa mujibu wa Sensa ya idadi ya watu na makazi ya 2022, asilimia 11 ya idadi ya Watanzania wote kuanzia miaka saba (7) na zaidi wana aina moja au nyingine ya ulemavu.

Kati ya wote wenye ulemavu, ulemavu wa kuona, kusikia, kuongea na kutembea ni asilimia sita na nusu (6.5), hii ni sawa na jumla ya watu 3,154,514 wenye ulemavu pasipo kujali dhehebu au dini ya muhusika. Kutokana hali zao watu hao wanahitaji mipango na mikakati maalum ya kuwafikia kwa huduma za kimwili, kijamii, kiafya na Kiroho pia.

Kwa kuwa Kanisa ni mshiriki muhimu katika maendeleo na ustawi wa jamii, Kanisa katoriki linatekeleza majukumu hayo sio tu kwa mujibu wa maelekezo ya kitabu kitakatifu na miongozo ya kanisa, bali pia sera, sheria na miongozo ya nchi, kanda na ulimwengu isiyokinzana na imani na mafundisho ya kanisa katoriki kama vile:

Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu (2004), inalenga kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu kwa kuhakikisha wanapata fursa sawa katika elimu, ajira, huduma za afya, na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi.

Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (2006): ambao unalenga kulinda haki na heshima ya watu wenye ulemavu,kuhakikisha usawa na kutokomeza ubaguzi katika nyanja zote za maisha.

Itaendelea ……………………………….

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *