Wajibu wa Kanisa kwa watu wenye ulemavu katika huduma za Kiroho

Na Angela Kibwana

Mpendwa msomaji katika mfululizo wa makala haya ya “wajibu wa kanisa kwa watu wenye ulemavu katika huduma za kiroho” Makala yaliyopita yalianza na kuonesha kwamba kanisa kama jumuiya ya waamini wanao mwamini Kristo, msingi wake ni Kristo mwenyewe ((Waefeso 5: 29; Wakolosai 1: 24 na Wakolosai 2:10).

Katika kulithibitisha hilo makala hayo yalionesha namna Yesu Kristo mwenyewe alivyo kasimisha majukumu yake  ya  kulihudumia kanisa  la hapa duniani  kupitia mtume Petro, na msingi huo huo ndiyo asili ya uwepo wa  kanisa Katoriki ((Mathayo 16:18).

Makala hayo yalisisitiza kwa kuwa Yesu Kristo ndiyo msingi wa kanisa, kanisa la duniani halina budi kuyaishi maneno, matendo pamoja na kuubeba wajibu ambao Yesu Kristo aliukasimisha kwa Kanisa la hapa duniani kama ilivyothibitishwa kupitia Bibilia Takatifu na mafundisho ya mama kanisa.

Makala hayo pia yalisisitiza kuwa kanisa kama jumuiya ya waamini wanaomwamini Kristo, waamini wake wanayo mahitaji tofauti ambayo ndiyo msingi wa ustawi wao kiroho na kimwili. Makala hayo yakaangazia ni kwa namna gani kanisa la hapa duniani linaweza au linayatafsiri mahitaji hayo katika utekelezaji wa majukumu yake kiroho na kimwili pasipo kumwacha muumini yeyote ambaye ni mwili na Kielelezo cha Kristo nje ya huduma hizo. “Waamini wenye ulemavu na mahitaji yao ya kiroho ndiyo ukawa msingi wa makala hayo”

Katika makala ya toleo hili tunaendelea kuangazia hali ya upatikanaji wa huduma za kiroho ndani ya kanisa katoriki kwa watu wenye ulemavu, pasipo kuyatenga makundi mengine ya watu wenye ulemavu makala haya yatajikita kwa undani zaidi kwenye vikwazo vya mawasiliano kwa kundi la watu wenye ulemavu wa kuongea na kusikia ili kuweka usawa wa kihuduma kiroho, kiafya, kijamii na kimtazamo pia.

Kutokana na takwimu za matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 nchini Tanzania, kati ya watu wote wenye ulemavu, ulemavu wa kuona, kusikia, kuongea na kutembea ni 6.5% ya Watanzania wote, ambayo ni sawa na jumla ya watu 3,154,514 kuanzia umri wa miaka saba (7)  na kuendelea pasipo kujali dhehebu au dini ya mhusika, kwa hiyo kutokana na hali zao watu hawa wanahitaji mipango na mikakati maalum ya kuwafikia kwa huduma za kimwili, kijamii, kiafya, kielimu na kiroho pia.

Ni muda muafaka sasa wa Kanisa la mahalia kujiuliza ni juhudi zipi zinafanyika kuwafikia watu (waamini) wenye ulemavu wa kusikia na kuongea  kwa kujifunza na kuimarisha miundo mbinu ya mawasiliano kupitia lugha ya alama na teknolojia ya mawasiliano ili kuhakikisha kundi hili linastawi kupitia huduma na  mafundisho ya imani ili kuponywa kiroho na kimwili kwa neno la Mungu kama Kristu mwenyewe alivyotekeleza jukumu hili akiongozwa na huruma na upendo.

Katika jamii nyingi, watu wenye ulemavu wakiwemo wenye ulemavu wa kusikia na kuongea wamejikuta wakisukumwa pembezoni mwa huduma za kijamii na za kiroho.

Mahitaji yao kutokuzungumzwa au kuwekewa mkazo kwa upana wake kijamii na kitaasisi,pamoja na kusisitizwa katika biblia takatatifu.

Jambo hili linamkumbusha kila mmoja wetu binafsi na katika mamlaka ya kitaasisi kuweza ku wajibika katika kulifikia kundi hili (Luka 14:12-13).

Wakati Kanisa linaadhimisha Ekaristi, kuimba nyimbo za sifa, na kushiriki mafundisho, watu wenye ulemavu wa kusikia na kuongea mara nyingi wanakosa nafasi ya kuelewa ujumbe wa wokovu.

Changamoto kama ukosefu wa miundo mbinu, wataalamu wa lugha ya alama na mitazamo potofu juu ya uwezo wao wa kushiriki kikamilifu katika uinjilishaji, masuala mengine ya kiroho na kijamii, imekuwa ni kikwazo kwao.

Katika baadhi ya makanisa, mafundisho ya kiroho, kama Katekisimu, yanaelekezwa kwa njia ambazo zinategemea mazungumzo ya sauti pekee, hali inayowaacha watu wenye ulemavu wa kusikia bila ufahamu wa kina wa imani yao.

Ziko baadhi ya Sakramenti ambazo zimekuwa si rahisi kuzipata, hasa sakramenti ya Kitubio, imekuwa ngumu kwa waamini wenye ulemavu wa kuongea na kusikia kwa sababu mara nyingi hakuna mfumo mbadala wa mawasiliano unaoweza kuhakikisha usiri na ufahamu wa pande zote mbili kati ya Padri na muungamaji.

Hata hivyo Yesu Kristo mwenyewe alikuwa ni mfano wa kuigwa katika kuyafikia makundi ya watu wenye ulemavu ili kuwajumuisha katika huduma za kiroho, kimwili na kijamii kama inavyothibitishwa katika maandiko matakatifu, tunaona jinsi Yesu alivyowapokea watu waliokuwa na mahitaji maalum kwa huruma na upendo mkubwa.  Mfano katika Marko 7:32-35, Yesu alimponya mtu kiziwi na mwenye kigugumizi, akimtenga na umati ili kuonyesha heshima na huruma ya kipekee. “Aligusa masikio na ulimi wa mtu huyo, akionyesha kwamba mawasiliano ya kweli yanahitaji kugusa maisha ya wengine kwa ukaribu na upendo wa dhati”.

Kwa kielelezo hiki, Kanisa lina nafasi ya kipekee na ya kiutume kulifikia kundi hili kama Yesu Kristo mwenyewe alivyofanya. Kanisa linaalikwa kuhakikisha kwamba hakuna mmoja wa kondoo wa Kristo anayepotea kwa sababu ya ukosefu wa mawasiliano “Enendeni Ulimwenguni mwote mkahubiri Injili kwa kila kiumbe” (Marko 16:15)

Kwa hiyo kujifunza lugha ya alama kuimarisha teknolojia ya mawasiliano, kuunda mazingira jumuishi ya ibada, na kushirikisha wataalamu wa mahitaji maalum ni hatua za kiutendaji zinazoweza kuleta mabadiliko kiimani na kiroho kwa watu wenye ulemavu.

Ni wajibu kwa kanisa, viongozi wote wa Kanisa na makuhani kuhakikisha wito huo wa huduma si chaguo bali ni jukumu lililoachwa wazi na Kristo mwenyewe, kuwahudumia wale walioko pembezoni kwa upendo na utu, wakijua kwamba kwa kufanya hiyo wanatekeleza agizo la Kristo (Luka 14:12-13)   na  wanamtumikia Kristo mwenyewe ( Luka 14:13 ).

Aidha suala la  Watu Wenye Ulemavu ni la kisera ( Sera ya Watu Wenye Ulemavu 2004) kama ilivyo elekezwa na kusisitizwa kuhusu umuhimu wa  kubuni mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu, ili kutoa huduma bora za afya, na kuwasaidia kupata elimu na ajira.

Sera hii inaelekeza kwamba huduma za elimu (Ikiwemo elimu ya dini/ neno la Mungu) na afya zifanyike kwa njia inayowafaa watu wenye ulemavu, ikiwa ni pamoja na kuwa na walimu na wataalamu waliobobea katika lugha ya alama na kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu wa kusikia.

Hata hivyo kwa upande wa Miongozo ya Elimu kwa Watu Wenye Ulemavu Serikali ya Tanzania imetoa miongozo ya elimu kwa watu wenye ulemavu ambayo inasisitiza kwamba elimu jumuishi lazima iweze kupatikana kwa watu wote, ikiwa ni pamoja na watu wenye ulemavu wa kusikia.

Miongozo hiyo inataka shule zote ziwe na walimu waliofundishwa lugha ya alama na vifaa saidizi  ili kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wa kusikia wanapata haki zao katika elimu,bila ubaguzi.

Moja ya mifano inayoweza kuonesha jinsi kundi la watu wenye ulemavu wa kusikia na kuongea lilivyoweza kusahaulika kiroho ni ile hali ya kutoandaliwa kwa ibada na mafundisho ya dini kwa ajili yao.

Kwa mfano, baadhi ya parokia na makanisa mara nyingi hufanya ibada na huduma za kiroho bila kuzingatia mahitaji maalum ya watu wenye ulemavu wa kusikia, Hii inajitokeza wazi pale ibada zinapoendeshwa bila matumizi ya lugha ya alama au vifaa visaidizi, na waamini wenye ulemavu wa kusikia na kuona hivyo wanakosa njia ya kuelewa mafundisho ya neno la Mungu, Maombi, sala na matukio ya kiibada.

Katika hali hii, watu hawa wanakosa uelewa wa neno la Mungu na mafundisho ya kidini ambayo ni muhimu kwao, watu wenye ulemavu wanakosa vitabu vya dini vinavyotafsiriwa kwa lugha ya alama au tafsiri maalum za mafundisho ya kidini kwa njia rahisi.

Ushahidi mwingine ni jinsi wanavyoshindwa kushiriki kikamilifu katika Sakramenti kwa sababu Katika maeneo mengi, huduma za Sakramenti kama ubatizo, kipaimara, kitubio na Ekaristi, hutolewa bila kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu wa kusikia wanapata mafundisho ya kutosha na wanashirikishwa kikamilifu.

“Kwa mfano, watoto wenye ulemavu wa kusikia mara nyingi hawapati mafundisho ya katekesi kwa njia inayowafaa, na hivyo kuathiri uwezo wao wa kuelewa na kushiriki katika mafundisho ya imani”.

Lengo la makala haya ni kuchunguza upungufu wa elimu kwa viongozi wa dini kuhusu umuhimu wa kuwasikiliza na kuwahudumia watu wenye ulemavu wa kusikia.

Mpendwa msomaji wa makala haya katika Injili ya Mt. Yohana 9:1-3Yesu alipokataa imani potofu kuwa ulemavu ni matokeo ya dhambi, alianzisha mtazamo mpya wa heshima kwa watu wenye changamoto za kimwili.

Kanisa linaitwa kufundisha jamii kuhusu mtazamo huu, likisisitiza kuwa watu wenye ulemavu ni wa thamani mbele za Mungu na wanastahili kushiriki kikamilifu katika maisha ya kiroho.

Kadhalika katika Injili ya Mt. Mathayo 15:30-31Yesu alipowaponya watu wenye ulemavu na makutano wakamtukuza Mungu, alionyesha kuwa miujiza yake ilikusudiwa kuimarisha imani ya jamii nzima, hivyo ujumbe huu unatoa somo kwa Kanisa kwamba huduma kwa watu wenye ulemavu inapaswa pia kuwa chombo cha kujenga umoja na imani ya waumini wote.

Ikiwa viongozi wa dini na waamini hawajafundishwa kuhusu umuhimu wa kujua lugha ya alama na namna ya kuwawezesha watu hawa kushiriki katika shughuli za kidini, ni rahisi kuona kuwa kundi hili linashindwa kufaidika kiroho kama ilivyo kwa waumini wengine.

Katika Agano la Kale kitabu cha Kutoka 4:11“Bwana akamwambia, Ni nani aliyeumba kinywa cha mwanadamu? Au ni nani afanyaye mtu kuwa bubu, au kiziwi, au mwenye kuona, au kipofu? Si mimi, Bwana?”

Kwa hiyo ujumbe huu wa neno la Mungu unakumbusha kuwa Mungu ndiye Muumba wa kila mtu, na kila mtu ana thamani kubwa mbele zake, bila kujali hali yake.
Katika Mambo ya Walawi 19:14“Usimlaani kiziwi, wala usitie kikwazo mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako. Mimi ndimi Bwana.”Hapa waamini na Kanisa mahalia linasisitizwa jinsi tunavyopaswa kuwachukulia  na kuwaonyesha upendo na utu wale wenye ulemavu, kama agizo la moja kwa moja kutoka kwa Mungu muumba wa dunia na viumbe vyote.

Hii ni hali inayoonyesha wazi kuwa, licha ya maendeleo katika nyanja nyingine za kitekinolojia, kijamii na kiuchumi, kundi la watu wenye ulemavu wa kusikia na kuongea limekuwa likisahaulika kiroho, hali ambayo inahitaji mabadiliko ya haraka.

Katika muktadha huo wa kukuza mafundisho ya Kiroho kwa watu wenye ulemavu, Kanisa linaalikwa kufuata mfano wa Yesu wa kutibu na kuwahudumia wale waliotengwa na jamii.

” Wakamwendea Makutano mengi  wakimletea viwete,vipofu, mabubu,vilema na wengine wengi, wakawaweka miguuni pake, naye akawaponya; hata makutano wakastaajabu walipoona mabubu wanena, viwete wanenda, vipofu wanaona; wakamtukuza Mungu wa Israeli.”Mathayo 15:30-31

Kazi ya Kristu katika kuhudumia watu wenye ulemavu imejidhirisha katika sehemu nyingi kwenye maandiko matakatifu na kazi hiyo aliifanya kwa huruma na upendo kwa hiyo ni wito kwa jamii kuepuka unyanyapaa kwa kundi hili muhimu

Tunaposoma maandiko Mtakatifu katika agano jipya Marko 7:32-35
Yesu alipomponya mtu kiziwi mwenye kigugumizi, alifanya hivyo kwa heshima na huruma.

Kitendo hiki ni mfano wa jinsi Kanisa linavyopaswa kuwahudumia watu wenye ulemavu: kuwajali, kuwatia nguvu, na kuwaunganisha kikamilifu katika jamii ya waamini.

Kwa upande wa Mwinjili Luka 7:22Yesu anapotaja viziwi kama sehemu ya kundi analowahudumia, anaonyesha kwamba huduma kwa watu wenye mahitaji maalum ni sehemu muhimu ya utume wa Kanisa.

Hii inatoa changamoto kwa viongozi wa Kanisa kujifunza lugha ya alama na mbinu nyingine za mawasiliano.

Naamini kwamba Kanisa na viongozi wa Kanisa wana nafasi muhimu na ya kipekee katika kutekeleza wajibu wao wa kiroho kwa watu wenye ulemavu wa kusikia na kuongea

Ili kuanzisha utekelezaji wa wajibu huu, ni muhimu kuzingatia hatua mbalimbali za kimafunzo, rasilimali,na ushirikishwaji wa kundi hili katika shughuli za kiroho

Pia ni muda muafaka kwa viongozi wa dini na waamini kutazama picha kamili ya idadi ya watu wenye ulemavu wanaoonekana katika nyumba za ibada hasa siku za dominika na maadhimisho mengine ya Kanisa, kama hawashiriki katika Misa swali la kujiuliza je wako wapi?

Itaendelea …………………………………..

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *